Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akizungumza wakati akifungua mkutano wa siku moja wa Tume na Wadau wa Uchaguzi uliofanyika leo Julai 24, 2024 Mjini Bukoba Mkoani Kagera.Wadau hao ni pamoja na Viongozi wa vyama vya siasa, Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wahariri wa Vyombo vya habari, Waandishi wa habari, Maafisa Habari wa Mikoa na Halmashauri, Wawakilishi wa Makundi mbalimbali ya Vijana, Watu wenye ulemavu, Wanawake na Wazee wa Kimila.
Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile akiwasilisha mada.
*******************
Na. Waandishi Wetu, Geita na Kagera
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mkoani Geita na Kagera utafanyika kwa siku saba kuanzia tarehe 05 hadi 11 Agosti, 2024 ambapo vituo vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele wakati akifungua mkutano wa wadau wa uchaguzi mkoani Geita leo tarehe 24 Julai, 2024.
Mkutano kama huo mkoani Kagera umefunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Juji Rufaa (Mstaafu) Mbarouk Salim Mbarouk. Mikutano hiyo inafanyika ikiwa ni maandalizi ya uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo.
“Mzunguko wa pili wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura utajumuisha mkoa huu wa Geita na Kagera ambapo uboreshaji utaanza tarehe 5 hadi 11 Agosti, 2024. Vituo vitafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa mikoa hiyo inafanya uboreshaji kwenye mzunguko wa pili baada ya mzunguko wa kwanza ambao umejumuisha mikoa ya Kigoma, Katavi na Tabora ambako uboreshaji umeanza tarehe 20 Julai, 2024 na unatarajiwa kukamilika tarehe 26 Julai, 2024.
“Tume tayari imeanza zoezi la uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura ambapo uzinduzi ulifanyika mkoani Kigoma tarehe 20 Julai, 2024 na mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB). Uzinduzi huo umeenda sambamba na kuanza kwa mzunguko wa kwanza wa uboreshaji kwenye mikoa mitatu ya Kigoma, Tabora na Katavi. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo unaendelea hadi tarehe 26 Julai, 2024,” amesema.
Akizungumza mkoani Kagera, Mhe. Jaji Mbarouk amesisitiza kuwa kadi za wapiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, amewataka wadau wa uchaguzi kwenye mkoa huo kuwaelimisha wapiga kura wenye kadi hizo wasiende kuboresha taarifa zao kwa kuwa zoezi hilo haliwahusu.
“Kwa mujibu wa kifungu cha 168 cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024 kadi za mpiga kura zilizotolewa mwaka 2015 na 2020 zenye jina la Tume ya Taifa ya Uchaguzi ni halali na zitaendelea kutumika kwenye chaguzi zijazo. Hivyo, zoezi hili la uboreshaji wa Daftari haliwahusu wapiga kura wenye kadi hizo,” Jaji Mbarouk amesema.
Akizungumzia teknolojia ya uandikishaji wa wapiga kura wakati wa kuwasilisha mada, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Kailima Ramadhan amesisitiza kuwa wapiga kura wanaoboresha taarifa zao wanaweza kuanza mchakato wa awali kwa kutumia simu janja au kiswaswa na kompyuta kupitia mfumo ujulikanao kama Online Voters Registration System (OVRS) au kwa kubobya *152*00#, kisha namba 9 na kufuata maelekezo.
”Mtumiaji wa huduma hii, atatakiwa kufika kituo anachokusudia kujiandikisha ili akamilishe hatua za kupigwa picha, kuweka saini na kupatiwa kadi yake ya mpiga kura,” amesema Bw. Kailima.
Meza kuu ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk (katikati) Mjumbe wa Tume, Mhe. Magdalena Rwebangira (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Uchaguzi ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile
Viongozi wa kimila ni miongoni mwa wadau muhimu wa Uchaguzi hivyo Tume iliwashirikisha viongozi hao kutoka Kagera.
Wadau kutoka makundi mbalimbali ya wanawake na vijana nao walishiriki.
Wahariri kutoka Vyomb0 vya habari nao walishiriki.
Vyama vya siasa nao walishiriki
Viongozi wa Dini nao walishiriki
Makamu Mwenyekiti Wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), Mhe. Mbarouk Salim Mbarouk akiongoza majadiliano wakati wa Mkutano huo.
Maswali na maoni mbalimbali yaliulizwa na kutolewa na wadau na kupatiwa majibu.Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura, Bi. Giveness Aswile akifafanua jambo.
Maswali na maoni mbalimbali yaliulizwa na kutolewa na wadau na kupatiwa majibu.
No comments:
Post a Comment