Na Ludovick Kazoka, Dodoma
Kwa mara ya kwanza, Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imefanya upandikizaji uloto kwa mgonjwa wa sikoseli ambaye anatofautiana kundi la damu na mchangiaji wake wa uloto, huduma ambayo hapo awali haikuwa ikifanyika.
Akiongea leo, Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Damu BMH, Stella Malangahe, ( Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Damu) amesema BMH kupitia kitengo chake cha Damu Salama sasa kina uwezo wa kuchakata uloto uliyotolewa na mchangiaji mwenye kundi tofauti la damu na mpokeaji ( mgonjwa) na hivyo kupandikizwa bila kuleta madhara yoyote katika mwili.
Utaalam huu unaojulikana kama Bone Marrow Manipulation- RBC Depletion ni utaalam unaofanywa na mashine maalum ( Apheresis machine) kwa kuchuja na kuchukua Uloto ulio kusudiwa kisha kumwekea mgonjwa ( kumpandikiza) uloto uliobakia.
"Mgonjwa huyu aliyepandikizwa pamoja na mchangiaji wake wanaendelea vizuri na tayari mgonjwa huyu ameonesha dalili nzuri za kuotesha uloto. Mwanzoni tulipoanzisha huduma hii ya upandikizaji uloto hatukuweza kupandikiza uloto kwa mgonjwa mwenye sikoseli anayetofautiana kundi la damu mchangiaji wake, lakini sasa kupitia utaalam huu BMH tunaweza kupandikiza uloto kwa wagonjwa ambayo wachangiaji wao wana makundi tofauti ya damu" amesema Dkt. Stella
Dkt Stella ametaja vigezo vingine wanavyozingatia katika upandikizaji uloto mbali na kundi la damu, ambalo sasa limepatiwa ufumbuzi ni pamoja na umri wa mgonjwa ( miaka 4 hadi 12), uwepo wa mchangiaji uloto mwenye ufanano wa kina saba na mgonjwa ( HLA matching) na hali nzuri ya afya ya mgonjwa na mchangiaji uloto.
BMH imekuwa hospitali ya kwanza nchini kutoa huduma hii kwa wagonjwa wa sikoseli na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoa huduma hii kwa wagonjwa wa sikoseli.
Huduma ya upandikizaji uloto kwa wagonjwa wa sikoseli ni huduma inayolenga kuondosha kabisa ugonjwa wa sikoseli na kumfanya mgonjwa kupona ugonjwa huu na kurejea katika uimara wa afya kama watu wengine wasiona ugonjwa huo. Huduma hii inaendelea kutolewa BMH kwa mafanikio makubwa na hivyo kuendelea kuleta matumaini kwa watanzania wengi, ikizingatiwa kuwa Tanzania ni nchi ya 4 duniani kwa kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wenye sikoseli.
No comments:
Post a Comment