NITAKUJA KUMKABIDHI MKANDARASI, UJENZI WA LAMI BARABARA YA OMURUSHAKA - KYERWA: BASHUNGWA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, July 6, 2024

NITAKUJA KUMKABIDHI MKANDARASI, UJENZI WA LAMI BARABARA YA OMURUSHAKA - KYERWA: BASHUNGWA



Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) imeshampata Mkandarasi wa kuanza Ujenzi wa barabara ya Omurushaka – Kyerwa kwa kiwango cha lami ambapo hivi karibuni atamleta Mkandarasi aliyepewa kazi hiyo kumtambulisha na kumkabidhi kwa wananchi ili kuanza Utekelezaji.


Ameeleza hayo katika mkutano wa hadhara wakati akizungumza na Wananchi wa Kata ya Ihanda na kueleza kuwa tayari Mkandarasi ameshaoneshwa eneo la kujenga Kambi ambapo amepima Maeneo mawili ya Ihanda na Nkwenda.


“Muda wowote nitarudi, nakuja kumkabidhi Mkandarasi anaanza kujenga barabara kiwango cha lami kuanzia Makao Makuu ya Kyerwa mpaka Omurushaka, amesema Bashungwa.




Bashungwa amefafanua kuwa barabara ya Omurushaka - Kyerwa itaunganisha nchi ya Tanzania na Uganda kupitia mpaka wa Murongo na itapita kwenye Wilaya mbili za Karagwe na Kyerwa hivyo ni barabara muhimu kiuchumi kwa kuwa inapita maeneo muhimu yenye uzalishaji mwingi wa kahawa, ndizi maharage ambapo wananchi watanufaika nayo.


Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imeshatenga Milioni 111 kupitia Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kwa ajili ya ukarabati wa barabara Kayanga – Kyerunga – Ihanda.


Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa amechangia kiasi cha shilingi Milioni 12 ili iweze kukamilisha ujenzi wa jengo la Zahanati ya Kata ya Ihanda na kusisitiza kuwa kazi zingine zilizobakia ziendelee ili kufikia mwaka 2025 zahanati ianze kutoa huduma kwa wananchi wa Kata hiyo.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Ihanda, Ladislaus Kamuhangire ameeleza kuwa mradi wa ujenzi wa Zahanati ya Ihanda ulianza mwezi Machi, 2023 ambapo hadi hivi sasa umefikia hatua ya kuezeka na ikikamilika itasaidia kutatua changamoto ya umbali wa upatikanaji wa huduma ya afya kwa wananchi wa kata hiyo kuzifikia Zahanati ya Kayanga na Hospitali ya Nyakanongo.


Aidha, amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutoa fedha za miradi ya maendeleo ambapo katika mwaka wa fedha 2023/2024 wamepata zaidi ya Milioni 95 kwa ajili ya matengenezo ya barabara zilizopo katika Kata hiyo.




No comments:

Post a Comment