Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kulia)
akipata maelezo kuhusu masuala ya usalama wakati alipotembelea Banda
la Wizara ya Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya
Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Anayetoa maelezo ni Afisa
Mwandamizi Afya na Usalama mahali pa kazi kutoka TANESCO, Nelson
Boniface.
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga (kulia)
akipata maelezo kuhusu Nishati Safi ya Kupikia katika Maonesho ya
Kimataifa ya Biashara yanayoendelea jijini Dar es Salaam. Anayetoa
maelezo ni Adelina Lyakurwa, Afisa MAsoko Mwandamizi kutoka TANESCO.
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Innocent Luoga
amewataka Wataalam katika Wizara ya Nishati na Taasisi zake kujikita
katika kufanya kazi kwa kasi, umakini na bidii ili kuwafikishia
wananchi nishati ya uhakika na kwamba hicho ndicho kiwe kipimo kikuu
cha kutangaza kazi za Wizara kwa wananchi.
Kamishna Luoga amesema hayo wakati alipotembea Banda la Wizara ya
Nishati na Taasisi zake katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara
(SABASABA) yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
“Sisi Wizara ya Nishati tumejipa changamoto ya kuongeza bidii zaidi ya
kufanya kazi na kutoa huduma bora kwani kwani Watanzania wanachotaka
ni nishati ya kutosha ikiwemo ya umeme bila kuwa na usumbufu wowote.”
Amesema Mha.Luoga
Ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya Rais, Dkt. Samia
Suluhu Hassan imeendelea kuhakikisha kuwa inatoa fedha za kutekeleza
miradi ya uzalishaji, usafirishaji, usambazaji umeme pamoja na miradi
mingine ya Nishati akitolea mfano mradi wa umeme wa Julius Nyerere
(JNHPP) unaotekelezwa kwa kiasi cha shilingi trilioni 6.5 ambao sasa
umefikia asilimia 98.
Ametaja baadhi ya miradi mingine ya kimkakati inayoendelea kutekelezwa
kuwa ni pamoja na ya usafirishaji umeme itakayounganisha Mkoa wa
Katavi na Kigoma kwenye gridi ya Taifa ambayo ni mradi wa usafirishaji
umeme kutoka Tabora hadi Katavi na Tabora hadi Kigoma pamoja na miradi
ya kuboresha upatikanaji umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara.
Kuhusu Maonesho ya SABASABA amesema “nimetembelea mabanda ya Maonesho
ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake na kuona jinsi Wataalam
wanavyohudumia wananchi kwa umahiri na kutoa huduma mbalimbali ikiwemo
za kuunganisha umeme, kuonesha wananchi kwa vitendo matumizi ya
nishati safi ya kupikia na kutatua changamoto mbalimbali ambazo
wananchi wanaziwasilisha.”
Ameeleza kuwa, Maonesho hayo ni muhimu kwani Serikali inapata wasaa wa
kutoa taarifa za utekelezaji wa majukumu yake kwa wananchi na pia
kupata mrejesho wa huduma inazotoa, suala ambalo ni muhimu katika
kupima utendaji kazi.
Kuhusu utekelezaji wa ajenda ya Nishati Safi ya Kupikia, Mha. Luoga
amewaasa wananchi kutumia nishati iliyosafi ambapo amewahamasisha
kutumia majiko ya umeme yanayouzwa kwa gharama nafuu, yanatumia umeme
kidogo na kupika chakula kwa muda mfupi ikiwa ni matokeo ya teknolojia
mpya iliyobuniwa na TANESCO kwa kushirikiana na kampuni ya TaTEDO na
SESCOM.
Aidha, amewataka wadau wa nishati hiyo kuhakikisha kuwa wanakuwa na
kanzidata itakayojumuisha masuala mbalimbali ikiwemo idadi ya wananchi
wanaotumia nishati iliyosafi, matumizi yake n.k ambayo itatumika kama
moja ya njia za kujitathmini katika utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa
Nishati Safi ya Kupikia na kuchukua hatua stahiki zitakazowezesha
mkakati huo kutekelezwa kwa ufanisi.
No comments:
Post a Comment