Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jensita Mhagama (Mb) Peramiho akipata taarifa ya ujenzi wa miundo mbinu ya ujenzi wa madarasa katika shule ya sekondari Mpitimbi kutoka kwa Mwalimu Mkuu Patrick Matembo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jensita Mhagama (Mb) Peramiho na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi Ndg. Thomas Masolwa (kulia) wakikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jensita Mhagama (Mb) Peramiho akisalimiana na Mkuu wa shule ya sekondari ya Mpitimbi Mwalimu Patrick Matembo alipotembelea kujionea maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa.
Na Mwandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jensita Mhagama (Mb) Peramiho amepongeza uongozi wa shule ya sekondari ya Mpitimbi, Maposeni na Jenista Mhagama kwa ufaulu mzuri wa wanafunzi wa kidato cha sita katika matokeo yaliyotoka hivi karibuni.
Waziri ametoa kauli hiyo leo tarehe 15/07/2024 katika ziara yake iliyolenga kujionea maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari ya Mpitimbi ambapo alipata nafasi ya kuzungumza na wanafunzi wa shule hiyo iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Songea vijijini katika Mkoa wa Ruvuma.
Waziri amesema, “shule hizo tatu zimeheshimisha sana jimbo la Peramiho na tumejipanga kuhakikisha tunawapongeza walimu na kuwapongeza wanafunzi wa shule hizi kwa heshima mliompa Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, heshima mliompa Mbunge na heshima mliompa Diwani na hili jambo tutalibeba kwa ukubwa wake.”
Tunataka kila mtu aone mafanikio ya jimbo hili kitaaluma kwa watoto wa kitanzania wote wanaokuja kusoma katika shule zetu.
Kazi tuliyonayo kupitia Halmashauri ya wilaya ni kuhakikisha tunajenga uzio katika shule ya sekondari Mpitimbi, shule ya sekondari Maposeni na shule ya sekondari Jenista Mhagama ili wanafunzi waweze kusoma kwa utulivu zaidi, alieleza.
“Waziri Mhagama amesema mipango wa baadae ni kufanya shule hiyo kuwa kituo cha elimu kwa kuanzisha shule ya msingi sambamba na wanafunzi wa sekondari wa kidato cha kwanza mpaka kidato cha sita,” alisema Waziri Mhagama.
Niwaombe viongozi wangu tuendelee kumpa ushirikiano Mkuu wa shule na walimu wanaofundisha katika sekondari hizi kwa sababu utendaji wao mzuri wa kazi unaonekana hivyo tukishirikiana nao wataendelee kufanya kazi vizuri.
Kwa upande wake Katibu Tawala wa Wilaya ya Songea Ndg. Mtela Mwampamba amesema Mkuu wa shule ya sekondari Mpitimbi ni mwalimu wa mfano ametekeleza ujenzi wa miundo mbinu ya elimu kwa wakati na kwa thamani ya fedha inayotambulika kwa muda mfupi na bila kuwa na malalamiko.
“Niwashukuru wananchi kwa kumpa ushirikiano Mkuu wa shule ya sekondari ya Mpitimbi, kwa mikakati mizuri, naomba Mkurugenzi Mtendaji ulete watendaji wengine wa serikali waje wajifunze mbinu za utekelezaji wa miradi kwa ubora unaotakiwa na kwa wakati,” alisema Ndg, Mwampamba
Awali uongozi wa Serikali ya wanafunzi wa shule ya sekondari Mpitimbi ukiongozwa na Mwanafunzi Catherine January ulitoa salamu za shukrani kwa Serikali kwa fedha zilizotolewa kusaidia miundo mbinu ya ujenzi wa madarasa.
“Tunatambua jitihada zako za kuhakikisha miundo mbinu hii inatengewa bajeti na fedha zainakuja kwa ajili ya utekelezaji, tunaomba usichoke kuangali shule hii,” alisema kiongozi wa wanafunzi.
No comments:
Post a Comment