Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi mwa Umma na Utawala Bora na Mbunge wa Jimbo la Kibakwe, Mhe, George Simbachawene amesema ujenzi wa mradi wa Mahakama ya Mwanzo ya Kisasa katika Kijiji cha Kinusi unaweka historia kwani sehemu inapojengwa ni eneo gumu kufikika hivyo itasaidia kuchagiza utawala bora kwa wananchi wa Jimbo la Kibakwe kwa ujumla.
Ametoa kauli hiyo leo katika Kijiji cha Kinusi kilichopo Kata ya Ipera, Halmashauri ya Wilaya ya Mpwapwa jijni Dodoma wakati wa tukio la kukakabidhi eneo hilo la ujenzi wa Mahakama kwa Mkandarasi.
Amesema mradi huo wa ujenzi wa Mahakama utakaogharimu shilingi Bilioni 1.1 hadi kukamilika kwake umekuja kwa wakati muafaka kwani wananchi hawatalazimika kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda kutafuta haki zao Wilayani Mpwapwa.
Mhe. Simbachawene ameongeza kuwa ujenzi wa jengo hilo unarudisha historia ya eneo hilo la Ipera kwani miaka ya 1952 kulijengwa Mahakama na Waingereza iliyoanza kufanya kazi huku aliyekuwa Chifu wa eneo hilo, Chifu Zaina Sechamule alitumika kama Hakimu.
" Kihistoria eneo hilo linajulikana kwa jina la Kwilondoo ndiko eneo ambako kulikuwa kunapatikana haki na ndilo eneo alikokuwa akiishi Chifu na huyu alikuwa ni Chifu mwanamke, hivyo leo ni siku ya kihistoria ya kukabidhi eneo la ujenzi wa mahakama ya kisasa’’ amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Amesema ujio wa mahakama hiyo itasaidia kutoa haki kwa zaidi ya wananchi wa Kata sita zilizopo katika eneo hilo huku akizitaja hata zile Kata za jirani za Wilaya ya Kilosa, Mkoani Morogoro zitanufaika pia
Awali Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel amesema ujenzi wa Mahakama hiyo utagharimu Sh. Bilioni 1.1 na utachukua muda wa miezi nane hadi kukamilika kwake.
Amesema ujenzi huo utaleta chachu katika maendeleo ya eneo hilo huku akisisitiza kuwa Mradi huo ni wa kihistoria kwa sababu Kinusi ni miongoni mwa maeneo ambayo wameyabainisha kuwa ni magumu kufikika.
" Naomba nimshukuru sana Mhe.Rais Samia Suluhu Hassan kutokana na msukumo mkubwa anaouweka kwenye mahakama hauelezeki kwa vile Mimi ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama na Mimi ndio Afisa Masuhuli ninajua ninachokimaanisha" amesisitiza Prof.Elisante
Naye, Mkandarasi wa Jengo hilo, Audax Contractors mara baada ya kukabidhiwa eneo hilo ameahidi kukabidhi jengo hilo ndani ya muda huku akikisitiza ataheshimu makubaliano ya mkataba na kuhakikisha kuwa atazingatia masharti yote katika ujenzi wa mradi huo.
No comments:
Post a Comment