Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inautaarifu Umma kuwa taarifa za VVU na UKIMWI zilizochapishwa kwenye chapisho linalojulikana kama "Sexual Behaviors and HIV Status: A Population-Based Study among Youths and Adults in Tanzania" ni za upotoshaji.
Taarifa hizo zimechapishwa na Mhariri wa jarida la 'Journal of Infectious Disease and Epidemiology Volume 7 | Issue 8' DOI:10.23937/2474-3658/1510224 la mwaka 2021 na kusambazwa katika mitandao ya kijamii.
Kupitia chapisho hilo, Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania imebaini kuwa takwimu zilizooanishwa zikionesha kiwango cha ushamiri wa Virusi Vya UKIMWI (VVU) nchini Tanzania kuwa ni 80% si za kweli.
Tanzania ina taratibu zake za kufanya ufuatiliaji wa mwenendo wa hali ya Virusi Vya UKIMWI (VVU) na UKIMWI. Sambamba na hilo, Tanzania hufanya tafiti za mara kwa mara hali ya VVU na UKIMWI nchini kila baada ya miaka mitano (5). Utafiti wa kwanza wa mwenendo wa VVU na UKIMWI ulifanyika mwaka 2003/2004 ambapo ushamiri wa VVU (HIV Prevalence) ulikuwa 7.0%. Uliufuata ni utafiti mwingine wa mwaka 2007/2008 ambapo ushamiri wa VVU ulikuwa 5.7%, mwaka 2011/2012 ushamiri wa VVU ulikuwa 5.1%, na mwaka 2016/2017 ushamiri wa VVU ulikuwa 4.9%. Ushamiri wa VVU umeendelea kushuka hadi 4.4% kupitia utafiti wa mwaka 2022/2023. Hadi sasa Tanzania inakadiriwa kuwa na takriban watu 1,600,000 wanaoishi na Virusi Vya UKIMWI.
Aidha, kwa kuzingatia Sheria ya Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) Na. 22 ya mwaka 2001 na marekebisho yake Na.6 ya mwaka 2015, pamoja na kanuni zake GN Na.145 za mwaka 2016, kama ya 18 inatoa mwongozo wa namna ya utoaji wa taarifa zinazoihusiana na mwenendo wa hali ya VVU na UKIMWI nchini.
Kwa muktadha huo, Mwandishi na Mchapishaji wa Jarida hilo walipaswa kuzingatia matakwa ya sheria husika katika utoaji wa takwimu kwa Umma.
Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS) inakemea upotoshaji na utoaji wa taarifa za VVU na UKIMWI zisizo sahihi kwa Umma.
No comments:
Post a Comment