MHE. SANGU ATOA RAI KWA VIONGOZI WA UMMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, August 24, 2024

MHE. SANGU ATOA RAI KWA VIONGOZI WA UMMA


Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu ametoa rai kwa Viongozi wa Umma kuwa waadilifu kwa kuwa wana dhamana ya kusimamia taasisi na kufanya maamuzi katika Utumishi wa Umma.

Mhe. Sangu ametoa rai hiyo Agosti 23, 2024 wakati alipofanya ziara katika ofisi Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyopo katika jengo la Maadili (Maadili House) Jijini Dodoma kwa lengo la kujifunza majukumu yanayotekelezwa na taasisi hiyo.

“Hakikisheni mnatumia Sheria, Miongozo na Kanuni katika kusimamia maadili ya Viongozi katika Utumishi wa Umma, maadili ndio kila kitu, iwapo hatutaweka msingi wa maadili vizuri utoaji wa huduma Serikalini hautokuwa na tija na malalamiko ya wananchi hayawezi kukoma amesisitiza Mhe. Sangu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anataka kuona wananchi wanapata huduma vizuri lakini baadhi ya viongozi wa umma wanashindwa kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma, hivyo kuathiri nia njema ya Rais.

Aidha amebainisha kuwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni taasisi muhimu sana kwa kuwa chimbuko lake ni Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 1977. Hivyo, wanatakiwa kufanya kazi kwa kiwango cha hali ya juu wakizingatia kwamba ni taasisi tegemewa kwa ustawi wa Taifa.

Aidha, amesema kuwa, Viongozi wa Umma wasipozingatia utalaam, uaminifu na kutimiza wajibu wao ipasavyo matokeo yake ni kuvunja Sheria, kuwa na mwenendo usioridhisha na kufanya matukio yenye athari na hasara kwa wananchi na taifa kwa jumla.

Awali, Kaimu Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa Umma Bw. Waziri Kipacha amebainisha kuwa moja ya changamoto kubwa katika usimamizi ni kwa baadhi ya viongozi wa umma ambao wamebainika kujaza taarifa zisizo sahihi kwenye matamko ya rasilimali na madeni, hivyo wamebaini mbinu za kisasa katika kufanya uchunguzi wa masuala ya kimaadili.

Aidha, amesema kuanzia Oktoba 2024, Viongozi wote watatakiwa kutumia mfumo wa Online Declaration System (ODS) unaopatikana kupitia tovuti ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kwa ajili ya kujaza taarifa za Matamko ya Rasilimali na Madeni na kuziwasilisha kwa njia mtandao.

“Sisi kama Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Tutakupa ushirikiano wa kutosha katika kutekeleza majukumu uliyopewa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema Bw. Kipacha.

Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina Ofisi Dodoma, Morogoro, Dar es Salaam, Arusha, Mwanza, Tabora, Mtwara na Mbeya ambazo zinaendelea na majukumu yake ikiwemo kuchunguza mwenendo na tabia za viongozi wa utumishi wa umma.

No comments:

Post a Comment