Prof. Ng’umbi aanika mafanikio ya TEWW - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, August 22, 2024

Prof. Ng’umbi aanika mafanikio ya TEWW


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi (katikati) na viongozi wengine (waliokaa) wakiwa katika picha ya pamoja na wafanyakazi wa taasisi hiyo waliopandishwa madaraja hivi karibuni mara baada ya mkutano wa wafanyakazi wa TEWW walioko jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umefanyika makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam, leo Agosti 22, 2024.

Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Prof. Michael Ng’umbi akiongea wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa taasisi hiyo walioko jijini Dar es Salaam (hawako pichani) leo Agosti 22, 2024, makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) walioko jijini Dar es Salaam wakifuatilia kwa makini moja ya wasilisho lililokuwa likitolewa wakati wa mkutano uliofanyika leo Agosti 22, 2024 makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam

Baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW), Naibu Mkuu wa Taasisi (Mipango, Fedha na Utawala), Dkt. Godfrey Mnubi (wa pili kulia) na Mkurugenzi wa Utafiti, Machapisho na Ushauri Elekezi, Dkt. Bellingtone Mariki (wa pili kushoto) wakifuatilia wasilisho la Mkuu wa Taasisi hiyo, Prof. Michael Ng’umbi (hayupo pichani) wakati wa mkutano wa wafanyakazi wa TEWW walioko jijini Dar es Salaam. Mkutano huo umefanyika leo Agosti 22, 2024 makao makuu ya TEWW mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam.

Baadhi ya washiriki wa mkutano wa wafanyakazi wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima walioko jijini Dar es Salaam wakifuatilia hoja zilizokuwa zikitolewa wakati wa mkutano uliofanyika makao makuu ya taasisi hiyo mtaa wa Bibi Titi Mohamed jijini Dar es Salaam leo Agosti 22, 2024.


Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam


Mkuu wa Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima (TEWW) Profesa Michael Ng’umbi ameeleza mafanikio ya taasisi yake katika kipindi cha miaka mitatu (3) ya Baraza la taasisi hiyo.

Ameyasema hayo leo Agosti 22, 2024 katika mkutano wa wafanyakazi wa TEWW walioko jijini Dar es Salaam uliofanyika makao makuu ya ofisi za taasisi hiyo zilizoko mtaa wa Bibi Titi Mohamed alipokuwa akitoa mrejesho wa masuala yaliyojadiliwa na kuelekezwa na Baraza la taasisi hiyo lililomaliza muda wake hivi karibuni.

Profesa Ng’umbi amesema kuwa kabla ya Baraza hilo kuundwa taasisi yake haikuwa na mradi wowote wa ujenzi, lakini kwa sasa ina miradi hiyo takribani kila mkoa wa Tanzania Bara, hatua inayoongeza fursa ya kupata elimu kwa wananchi.

Kiongozi huyo aliyataja mafanikio mengine kuwa ni kwa taasisi hiyo kupata hati safi ya ukaguzi wa hesabu kwa miaka sita (6) mfululizo; kujazwa kwa nafasi za uongozi wa taasisi; na watumishi takribani 72 kupandishwa madaraja.

Sambamba na mafanikio hayo ni kuendelea kutekelezwa kwa ufanisi kwa miradi ya kuboresha elimu ya sekondari kwa wanafunzi wa kike wanaojiunga na elimu nje ya mfumo rasmi (SEQUIP-AEP); na mpango wa elimu changamani kwa vijana walio nje ya mfumo rasmi (IPOSA).

Mkuu huyo wa Taasisi aliwataka wafanyakazi kujipongeza kwa mafanikio yaliyofikiwa na kuendelea kufanya kazi pasipo kusukumwa, kutii maelekezo, na kuwa waadilifu wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.

Aidha, Profesa Ng’umbi aliueleza mkutano kuwa Baraza liliridhia azma ya taasisi hiyo ya kuwa na mkataba wa mashirikiano na Jeshi la Magereza katika kufungua vituo vya mafunzo magerezani; kuwajengea uwezo maafisa magereza kufundisha watu wazima; na kushirikiana katika masuala ya ujenzi na ukarabati wa majengo.

Pia, mkutano ulielezwa kuwa Baraza lilielekeza watumishi wanaochafua taswira ya taasisi, hususan katika eneo la mitihani waadhibiwe, na taasisi iongeze juhudi katika kuongeza mapato yake kwa kukusanya madeni.

Vilevile, ilielekeza pendekezo la maboresho ya Sheria ya TEWW Sura ya 139, toleo la 2002 liendelee kufanyiwa kazi kwa kuzingatia maoni ya wadau.

No comments:

Post a Comment