TANROADS YAKARIBISHA WANANCHI KUPATA ELIMU MAONESHO YA NANENANE DODOMA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Monday, August 5, 2024

TANROADS YAKARIBISHA WANANCHI KUPATA ELIMU MAONESHO YA NANENANE DODOMA


Na Okuly Julius, Dodoma


Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) imewataka wananchi kuacha tabia ya kuvamia maeneo ya hifadhi ya barabara ili kuepukana na madhara yanayoweza kujitokeza.

Hayo yameelezwa leo Agosti 5,2024 na Mhandisi wa Miradi ( TANROADS), Fulgence Lendo, wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda la TANROADS lililopo katika Maonesho ya Kilimo ya Kimataifa (Nane Nane) 2024 yanayofanyika Kitaifa Mkoani Dodoma.

Mha. Lendo amesema kuwa TANROADS wanatumia maonesho haya kutoa elimu ya uhifadhi wa barabara na athari za kujenga makazi katika hifadhi ya barabara na pia kuonesha baadhi ya mitambo inayotumika maabara kupima ubora wa lami inayotumika wakati wa ujenzi wa barabara.


"Wakala ya Barabara katika maonesho haya tunatoa elimu ya namna ya uhifadhi wa barabara, namna tunavyopima ubora wa barabara wakati wa ujenzi na baada ya kukamilika, kwa sasa hivi tuna mitambo ya kisasa ambayo Rais Samia ametupatia fedha na tumenunua ili kuhakikisha ubora wa barabara unazingatiwa, " amesema Mha. Lendo.

Ameongeza kuwa ..."tunawashauri wananchi juu ya athari zinazotokana ya wao kuvamia katika hifadhi ya barabara kuwa wanasababisha kupungua kwa upeo kwa madereva na kusababisha ajali kwa watembea kwa miguu na kwa magari mengine; na muda mwingine inahatarisha usalama wa watoto kwani wanacheza karibu na barabara hivyo niwashauri wanachi kuacha tabia ya kuvamia hifadhi ya barabara, " ameeleza Mhandisi Lendo

Pia amesema wanachi wanaotembelea banda hilo wanapata wanaoneshwa mtandao mzima wa barabara nchini ili wanaposafiri au kusafirisha bidhaa zao kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine wajue ni barabara gani inakuwa rahisi kufika wanapotaka kwenda kulingana na eneo walilopo


Kwa upande wake Mtaalamu wa Malighafi na Majenzi Barabara, Mhandisi Christina Luhwaga ameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuwawezesha TANROADS kupata vifaa vya kisasa, ambavyo vinahakisi utendaji wa kazi kwa kuangalia ubora wa Malighafi inayotumika katika ujenzi wa barabara kabla ya kufika eneo la ujenzi baada ya kujiridhisha na ubora wake.


Naye Fundi sanifu Mwandamizi wa TANROADS, Kitengo cha Utafiti na Maendeleo, Clement Ndagiwe amesema mitambo iliyotolewa na Serikali inawasaidia kujiandaa na matengenezo ya dharura, haraka na matengenezo ya muda mrefu kutokana na uchakavu wa barabara

"Mitambo hii inatusaidia kufuatilia maendeleo ya barabara na watumiaji kuendelea kufurahia usafirishaji na usafiri kwa kutumia barabara zetu," amesema Ndagiwe.


No comments:

Post a Comment