TANZANIA KUFANYA TATHMINI MALEZI MBADALA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, August 6, 2024

TANZANIA KUFANYA TATHMINI MALEZI MBADALA


WMJJWM- UGANDA


Serikali ipo katika mchakato wa kufanya tathmini ya huduma za Malezi mbadala na kuandaa mkakati wa kitaifa wa kuimarisha huduma za Malezi Mbadala.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha hayo Agosti 06, 2024 akiwa nchini Uganda, wakati wa ziara yake nchini humo yenye lengo la kujifunza utekelezaji wa mipango na mikakati dhidi ya watoto walio katika Mazingira hatarishi hususani afua za malezi mbadala.

Amesema, watoto walio katika mazingira hatarishi ni changamoto inayokabili nchi za Afrika Mashariki ambapo, Tanzania pia inakabiliwa na watoto hao ambao wanatambuliwa kila mwaka na kupatiwa huduma. 

"Takwimu zinaonesha kuna vituo 3,863 vilivyosajiliwa kulea watoto mchana vyenye jumla ya watoto 397,935 ambapo, kati ya vituo hivyo 206 ni vya kijamii. Aidha, maombi ya usajili wa vituo hivyo yameendelea kuongezeka ambapo, kwa mwaka wa fedha wa 2023/24 vimesajiliwa vituo 829. Kwa mwenendo huu, iko haja ya kuimarisha utaratibu utakaowezesha watoto kupata malezi mbadala." amesema Waziri Dkt. Gwajima.


Waziri Dkt. Gwajima ameongeza kwamba, Uganda ni kati ya nchi zilizochukua hatua za kufanya maboresho ya kuhudumia watoto walio kwenye mazingira hatarishi kwa kuimarisha huduma za malezi mbadala. Hivyo, ziara hiyo ni moja ya fursa ya kufanya tathmini yenye tija kwa kufanya ulinganifu wa namna Serikali ya Uganda ilivyoboresha huduma zao za malezi mbadala. 

Aidha, Tanzania inatarajia kupata uzoefu wa Uganda katika utekelezaji wa mikakati, na Sera unaoleta mabadiliko ya mfumo wa malezi mbadala ambayo yamekuwa yenye ufanisi, kujifunza mbinu zilizotumiwa katika kumarisha ulinzi na malezi ya watoto ngazi ya familia na namna Serikali ya Uganda inavyokabiliana na changamoto ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.

Ameendelea kusema kuwa, ziara hiyo itainufaisha Tanzania katika masuala ya kuimarisha ulinzi na usalama wa watoto hususani walio katika mazingira hatarishi na kupelekea kuimarisha afua za malezi mbadala ikiwemo makao ya watoto, programu ya walezi wa kuaminika, malezi ya kambo na kuasili na masuala ya watoto wanaoishi na kufanya kazi mtaani.

Katika ziara hiyo, Waziri Dkt. Gwajima ameambatana na Katibu Mkuu Dkt. Seif Shekalaghe, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera Mhando, Mwakilishi wa Ofisi ya Rais TAMISEMI, wataalamu na Wadau kutoka Umoja wa Familia kwa Watoto wote ambao wanashirikiana na Serikali kutekeleza afua za Malezi mbadala.

No comments:

Post a Comment