Na Angela Msimbira TARIME
Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya watu wazima, elimu nje ya mfumo rasmi,elimu maalum na michezo Ofisi ya Rais TAMISEMI , Ernest Hinju amekabidhi bendera ya Tanzania kwa timu za Wanafunzi, Walimu na viongozi wanaoshiriki Mashindano ya 22 ya michezo ya shule za Msingi na Sekondari ya Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (FEASSSA) yanayofanyika nchini Uganda.
Akikabidhi bendera hiyo leo Agosti 16, 2024 kwenye Chuo cha Ualimu Tarime Mkoani Mara Hinju amewataka Wanafunzi, Walimu na Viongozi wanaoenda kushiriki Mashindano hayo kujituma na kutumia umahiri wao kwa kila mchezo huku wakitambua kuwa wanaliwakilisha Taifa la Tanzania katika mashindano hayo.
Aidha, Hinju amesisitiza upendo, umoja na mshikamano kwa washiriki wa michezo hiyo ambayo itashirikisha nchi mbalimbali ikiwa ni pamoja na Tanzania, Rwanda, Burundi, Kenya na Uganda.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuanza mnamo tarehe 17-27 Agosti 2024 katika mji wa Mbale, Uganda ambapo Tanzania itashiriki katika michezo ya Soka, Mpira wa Kikapu, Mpira wa Wavu, Hockey, Tennis, Riadha, Mpira wa Mikono na Netboli.
No comments:
Post a Comment