Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) amewasilisha taarifa ya hali ya huduma ya maji kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira.
Taarifa hiyo ilihusu majiji sita ya Dodoma, Dar es Salaam, Mbeya, Tanga, Arusha na Mwanza.
Mhe. Aweso amesema serikali inaendelea na jitihada mbalimbali kuhakikisha huduma ya maji katika majiji hayo inaboreshwa zaidi. Jitihada hizo zinahusisha kupanua mtandao wa usambazaji maji kuanzisha na kukamilisha miradi inayoendelea ili kuhakikisha eneo lote la majiji hayo linafikiwa na huduma ya maji.
Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji wa Kiwira ambao unatarajia kugusa eneo kubwa la jiji la Mbeya, mradi wa Maji wa Butimba jijini Mwanza, mradi wa kuboresha huduma ya maji katika jiji la Arusha ambao umegharimu zaidi ya shilingi Bilioni 520 pamoja na miradi mingine mikubwa na midogo.
Amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha jitihada zinazofanywa na wizara zinapata msukumo wa kutosha ili kufanikisha lengo la "kumtua mama ndoo ya maji'
Kamati hiyo imeongozwa na Mwenyekiti wake Mhe. Jackson Kiswaga (Mb) ambaye amesisitiza Wizara ya Maji kuhakikisha inatekeleza maagizo ya serikali ambayo ni pamoja na kusikiliza kero za wananchi.
No comments:
Post a Comment