Katika picha ni Watendaji mbalimbali wa Serikali na pamoja na Waumini walioshiriki katika ibada ya shukrani ya ujenzi wa Kanisa la Anglikana la Mt. Mariamu Lituhi wilaya ya Nyasa mkoani Ruvuma. |
Na Wandishi wetu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama ametoa wito kwa Wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuhakiki kumbukumbu zao katika Daftari la kudumu la Mpiga Kura.
Waziri ametoa kauli hiyo wakati alipomuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa, leo tarehe 04/08/2024 katika ibada ya shukrani ya ujenzi wa Kanisa la Mtakatifu Mariamu Lituhi - wilaya ya Nyasa, Mkoani Ruvuma.
Amewaomba wananchi kutumia haki yao ya kikatiba ya kuchagua au kuchaguliwa kwa yeyote mwenye sifa za kushirikina na wananchi kuongoza, kutosita kuomba kuchaguliwa.
Waziri amesema, “tuendelee kuiweka nchi yetu kwenye maombi, tumlilie Mungu tuvuke salama kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na tuvuke salama kwenye Uchaguzi Mkuu ili Tanzania iendelee kubaki kuwa kisiwa cha Amani.”
Ameongeza kusema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, inatambua mchango wa Kanisa Anglikana Tanzania katika Maendeleo ya Taifa letu Kiuchumi, Kisiasa na Kijamii.
Aidha Waziri Mhagama ametumia tafakari ya ujumbe wa Mungu kupitia kinywa cha Nabii Hagai sura ya kwanza, aya ya nane (Hagai 1:8) aliposema, “Sasa, basi, nendeni milimani mkalete miti, mlijenge upya hilo hekalu, nipate kulifurahia na kutukuzwa”.
Awali katika taarifa ya risala iliyosomwa na Bi, Shukrani Eliya Kilumbo alisema ujenzi wa kanisa ulianza Mwaka 2011 na mpaka sasa kimetumika kiasi cha Millioni 84 na inakadiriwa kiasi cha shilingi milioni 150 zinahitajika ili kukamilisha ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mt. Mariamu.
Tunashukuru taaisisi mbalimbali na watu wote ambao wako hapa kwa kazi hii kubwa ya kuitikia wito wa Mwenyezi Mungu aliowaagiza kupitia ujumbe wa Mtume Paulo kwa wafilipi 4,8;9
Katika ibada hiyo ya shukrani kiasi cha Milioni 52,300,000 kilikusanywa ikiwemo fedha taslimu na ahadi zitakazosaidia katika ujenzi wa kanisa la Anglikana la Mt, Mariamu Lituhi katika wilaya ya Nyasa.
No comments:
Post a Comment