Aweso aishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mkubwa katika kazi za Sekta ya Maji - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Tuesday, September 3, 2024

Aweso aishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano mkubwa katika kazi za Sekta ya Maji


Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb) ameishukuru Benki ya Dunia kwa ushirikiano wake mzuri na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Maji. Ametoa shukrani hizo akifunga mafunzo ya wiki tisa yaliyofadhiliwa na Benki ya Dunia kwa kuzijengea uwezo Mamlaka za Maji ili kuwa na sifa ya kupata Mikopo kutoka taasisi na mashirika mbalimbali ya fedha, kwa lengo la kusukuma mbele maendeleo ya Sekta ya Maji nchini.

Amesema, mafunzo hayo yamehusisha idadi ya Wataalam 40 kutoka Sekta ya Maji na yamewawezesha kuwa na uwezo na mbinu mpya za ushawishi kwa taasisi za fedha ikiwemo uandishi bora wa maandiko na usimamizi wa miradi, kupunguza upotevu wa maji, kupanga mipango bora na endelevu, kukusanya mapato na hatua mbalimbali ambazo zitawezesha maendeleo yaSsekta ya Maji na hivyo kuondoa utegemezi wa fedha kutoka Serikalini.

Amesema Benki ya Dunia imekuwa mshirika muhimu katika maendeleo ya Sekta ya Maji ikiwemo miradi ya maji ambayo inatekelelezwa kupitia Program ya Lipa Kutokana na Matokeo (PfoR). Aidha, ameiomba Benki hiyo kupanua wigo wa mpango wa PfoR ili uweze kusaidia maendeleo ya Sekta ya Maji katika Mamlaka za Maji nchini ambapo programu hiyo inagusa zaidi miradi ya maji ya vijijini inayosimamiwa na Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA).
Naye Mwakilishi wa Benki ya Dunia , Tanzania Bi. Ruth Kennedy Walker ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa ushikiano mkubwa katika kazi mbalimbali hususan katika Sekta ya Maji. Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwapa wigo mpana wa kupata fedha katika vyanzo mbalimbali vya fedha ambapo Benki za Biashara ndiyo watoaji wakubwa wa fedha za mikopo ila huitaji andiko lenye ushawishi.

Kwa upande wake Mhandisi Humphrey Mwiyombela ambaye ni mmoja wa washiriki waliopata mafunzo hayo amesema mafunzo yamekuja katika muda muafaka ambapo Wizara ya Maji inatekeleza Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji Awamu ya Tatu (WSDP III) ambayo pamoja na mambo mengine inalenga kuwezesha upatikanaji wa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi.

Mafunzo hayo yamewezesha kushirikishana uzoefu katika utatuzi wa changamoto mbalimbali ikiwemo utatuzi wa migogoro katika maeneo ya kazi, kupunguza upotevu wa maji na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa miradi ya maji, pia kuzingatia gharama.

No comments:

Post a Comment