Na Said Njuki, Arusha
MWENYEKITI wa Bodi ya Asasi za Kiraia (AZAKI) Mercy Silla amewataka wadau wa asasi hizo kutafuta jinsi ya kupunguza utegemezi kwa wafadhili hususani kutoka nje ya nchi.
Amesema ni wakati wa viongozi wa asasi za kiraia nchini kuangalia watakavyoweza kujitegemea katika kuendesha program mbalimbali za kijamii bila kutegemea misaada hususani kutoka nje ya nchi.
Silla alisema hayo juzi wakati akifunga wiki ya AZAKI iliyofanyika Jijini Arusha, ukishirikisha wadau zaidi ya 500 huku mada mbalimbali zikiwasilishwa na kujadiliwa sanjari na majibu ya maswali kadha wa kadha kujibiwa.
"Ni wakati sasa kwetu kuangalia namna nyingine kuweza kuendesha progaram zetu kwa kutotegemea misaada mingi kutoka kwa hisani wa nje, itakuwa vizuri tukapunguza utegemezi huo".alisema Silla.
Katika hatua nyingine alisema ni wajibu wa AZAKI kuhakikisha wanakuwa mstari wa mbele kuongeza ushiriki wa kutosha katika shughuli mbalimbali za kijamii kwa kuwashirikisha vijana.
“Tuhakikishe sasa vijana wetu wananufaika na fursa za kibiashara sambamba na kuwajengea uelewa wa kutosha ili kuwaboreshea uwezo wa ubunifu katika nyanja mbalimbali.
Alisema wiki ya AZAKI imeweza kuongeza uelewa wa kwa vijana hivyo kuweza kuzitambua haki zao ikiwa ni pamoja na kwamba wapo wengi waliopata elimu ya kuweza kuchangamkia fursa kadhaa zilizopo nchini kupitia kikoa hicho.
Kwa upande wake Mratibu wa mabadiliko ya tabia nchi wa Shirika la Action Aid Happy Itroz alisema kuwa kuna haja ya elimu kutolewa zaidi kuhusu maswala ya kilimo ikolojia kwani bado sekta ya kilimo nchini haijapewa kipaumbele cha kutosha.
Aliwataka mabenki ya ndani na nje kuhakikisha yanatoa mkopo wa riba nafuu kwa wakulima hivyo waweze kunufaika na mikopo nafuu ili kuboresha kilimo chao na kuondokana na kilimo cha mazoea.
No comments:
Post a Comment