CBCC YATAKIWA KUONGEZA NGUVU MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, September 13, 2024

CBCC YATAKIWA KUONGEZA NGUVU MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI


Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji ametoa wito kwa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo (CBCC) kuongeza nguvu katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Amesema changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ni kubwa hivyo, ni muhimu kuchukua hatua kuhakikisha dunia inakuwa salama. Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji amesema hayo alipokutana na Ujumbe kutoka Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Congo na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, ulioongozwa na Waziri wa Mazingira wa Jamhuri ya Congo Mhe. Arlette Soudan–Nonault jijini Dar es Salaam Septemba 12, 2024.

Dkt. Kijaji amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo, Tanzania imekuja na biashara ya kaboni ambayo pamoja na mambo kadhaa inahusisha upandaji wa miti ambayo hunyonya hewa ya ukaa.

“Sisi kama taifa tumeanza kuchukua hatua kwenye biashara ya kaboni na tunatamani tuungane, tushirikiane na tunufaike kwa pamoja kubadilishana ujuzi ili tufikie malengo, tunahitaji maendeleo ambayo wenzetu wamepiga hatua huku wakiharibu mazingira na waathirika wakubwa ni sisi nchi zinazoendelea,” amesema.

Kadhalika, Mhe. Dkt. Kijaji amepongeza CBCC kwa kukubaliana namna wanavyoweza kuzisaidia nchi wanachama kupata fedha ambazo tayari zimewekwa katika Mfuko wa Bluu na benki mbalimbali wanazofanya nazo kazi kwa ajili ya kuendeleza shughuli za utalii na mabadiliko ya tabianchi.

Aidha, katika kikao hicho, Tanzania, Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo na Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo zimekubaliana kuendeleza ushirikiano wa karibu ili kuimarisha juhudi za mazingira za kikanda na kukuza suluhu za pamoja kwa mabadiliko ya tabianchi na uhifadhi wa utofauti wa kibaiolojia katika Bonde hilo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Kijaji kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, amepokea Hati ya Makubaliano (MoU) ya Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, ambayo ataiwasilisha kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa hatua zaidi.

Kwa upande wake Waziri Nonault ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Tabianchi ya Bonde la Kongo ameshukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka Tanzania.

Hivyo, ameahidi kuwa timu ya wataalamu wa Mfuko wa Bluu wa Bonde la Congo, chini ya Makamu wa Rais wa Benki ya Maendeleo ya Nchi za Kati za Afrika (BDEAC) na Msimamizi Mkuu wa Shughuli za Utawala wa kamisheni, Jean Paterne Megne Ekoga itarejea hivi karibuni kwa ajili ya kushirikiana katika upembuzi wa miradi ya kipaumbele ambayo itapata fedha na kuanza utekelezaji.

No comments:

Post a Comment