Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Klabu za michezo za wizara na idara za serikali Tanzania, zitashiriki kwenye michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali Tanzania (SHIMIWI), inayotarajia kuanza kutimua vumbi tarehe 20 Septemba, 2024, kwenye viwanja mbalimbali mkoani Morogoro.
Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa, Daniel Mwalusamba alisema hayo leo tarehe 19 Septemba, 2024 mjini Morogoro kuwa tayari maadalizi yote muhimu yamekamilika, ikiwemo kukutana na viongozi na wachezaji wa klabu zinazoshiriki
Mwalusamba alisema michezo hiyo itafunguliwa rasmi tarehe 25 Septemba, 2024 na Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati , Dk Doto Biteko .
“Hii ni michezo inayoshirikisha watumishi wa umma tunawakaribisha wananchi na wakazi wa mkoa wa Morogoro na watumishi wa umma wote muungane nasi katika kutazama vipaji kutoka kwa watumishi wa umma kwa siku zote 18 tutakazokuwa hapa, alisema Mwalusamba.
Hatahivyo, Mwenyekiti huyo amesisitiza umuhimu kwa watumishi wa umma wanaoshiriki michezo hiyo kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya utumishi wa umma kwa siku zote 18 watakazokuwepo kwenye kituo cha michezo.
Tumetoka kwenye vituo vyetu vya kazi mikoa mbalimbali na kwa sasa tumehamisha tu vituo vyetu vya kazi kwenye michezo hapa Morogoro, inatupasa kuendelea kuzingatia kanuni, taratibu na maadili ya kiutumishi wa umma ya kuwa na nidhamu tunapokuwa michezoni na nje ya michezo, haitapendeza kusikia klabu moja inawazomea wenzao kwa namna ambayo sio nzuri tuwe na staa kwenye ushangiliaji na haitapendeza kufanya vurugu mkiwa nje ya viwanja aidha kwenye hoteli tulizofikia, alisisitiza Mwalusamba.
Halikadhalika, amewataka viongozi waliopewa dhamana na waliokuja na timu zao kuwasimamia watumishi waliopo katika michezo hiyo kuhakikisha wanakuwepo kambini baada ya michezo, kuwepo viwanjani kila wanapotakiwa kucheza na kuangalia afya zao.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa SHIMIWI, Alex Temba ameitaja michezo itakayoshindaniwa kuwa ni pamoja na mpira wa netiboli, mpira wa miguu, mbio za baiskeli, kuvutana kwa kamba, karata, riadha , bao, darts (vishale) na drafti.
Temba alisema viwanja vitakavuotumika kw ajili ya michezo hii ni pamoja na Jamhuri, Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) vilivyopo katika Kampasi ya Edward Moringe ( Kampasi Kuu) na Kampasi ya Solomon Mahlangu ( Mazimbu), Shule ya Sekondari ya Morogoro na Chuo cha Teknolojia ya Ujenzi ambapo zamani kikijulikana Chuo cha Ujenzi..
Kwa sasa tuinawasisitizia klabu kuhakikisha wanakamilisha usajili wa timu zao ili mashindano haya yafanyike katika ubora na viwango vilivyokusidiwa, ambapo pia Baraza la Michezo la Taifa watakuwepo katika mashindano hayo kwa ajili ya kukamilisha usajili wa vilabu ambavyo haijafanya hivyo kwa lengo la kuifanya michezo hiyo iweza kufanya kazi na iendane na taratibu za kiserikali, alisema Temba..
Alisema kaulimbiu ya michezo hii ni “Michezo Huboresha Utendaji Kazi, Shiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa Ujenzi wa Taifa Endelevu’
Temba alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk Samia Suluhu Hassan, katika kuendeleza michezo na kwamba ameahidi kuwa wakiwa kama watumishi wa umma watashiriki kikamilifu uchaguzi wa serikali za mitaa bila kukosa.
No comments:
Post a Comment