
Na Okuly Julius, OKULY BLOG, DODOMA
Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Watu Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga, amewapongeza watumishi wa Ofisi hiyo kwa juhudi zao za kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano, akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo.
Akizungumza Machi 17, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Ofisi hiyo, Nderiananga amesema Ofisi ina imani kubwa na watumishi wake katika kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kujituma.
Ameeleza kuwa mabaraza ya wafanyakazi yameanzishwa kwa lengo la kuongeza tija na ufanisi mahali pa kazi, sambamba na kutoa jukwaa la wazi kwa watumishi na waajiri kubadilishana mawazo, kufanya majadiliano yenye tija na kuimarisha ushirikiano kwa manufaa ya taasisi na wafanyakazi kwa ujumla.
Nderiananga amesisitiza kuwa majadiliano yanayofanyika katika mkutano huo yanapaswa kulenga kuimarisha utendaji kazi wa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
“Ofisi yetu ina utaratibu wa kufanya mikutano hii kwa sababu inasaidia kujadili bajeti kwa pamoja, ambapo watumishi wanapata nafasi ya kuiridhia na kuipitisha kabla ya kuwasilishwa Bungeni. Hivyo, mabaraza haya ni muhimu sana kwetu,” amesema Nderiananga.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Dkt. Jim Yonazi, amewashukuru wajumbe wa Baraza kwa kujitolea na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Dkt. Yonazi amesema mkutano huo utajadili agenda kuu ya bajeti pamoja na kupitia taarifa ya utekelezaji wa bajeti kabla ya kupitishwa rasmi.







No comments:
Post a Comment