OPERATION KISIWANI GANA: DC NGUBIAGAI NA MBUA WAFUTILIA MBALI NYAVU HARAMU ZA SH. MILIONI 73 - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Friday, June 19, 2026

OPERATION KISIWANI GANA: DC NGUBIAGAI NA MBUA WAFUTILIA MBALI NYAVU HARAMU ZA SH. MILIONI 73


Na: Mwandishi Wetu, OKULY BLOG, UKEREWE 


Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe, Cde. Christopher Ngubiagai, amedhihirisha uzalendo wake wa hali ya juu kwa kuongoza operesheni kabambe ya kuteketeza zana haramu za uvuvi zenye thamani ya shilingi milioni 73,615,000.

​Shughuli hiyo muhimu ilifanyika mnamo Juni 18, 2026, katika kisiwa cha Gana kilichopo kijiji cha Kamasi, Kata ya Ilangala, ikiwa ni sehemu ya mikakati madhubuti ya kulinda rasilimali za Ziwa Victoria.


​Katika kuonyesha dhamira yake thabiti ya kulinda uchumi wa taifa, Cde. Ngubiagai amesisitiza umuhimu wa jamii kuachana na mbinu haramu za uvuvi zinazoharibu mazalia ya samaki.

​Kiongozi huyo amewahimiza wananchi kuongeza thamani ya mazao ya samaki kupitia usindikaji na uhifadhi bora badala ya kutegemea mauzo ya samaki pekee.


​Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Ndg. Vicent Mbua amewapongeza wananchi na wajumbe wa kamati kwa ushirikiano wao wa dhati, hatua ambayo inachochea ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo katika ushiriki wa zoezi hilo. 

Amesema, ili kukuza mapato ya halmashauri, kila mvuvi azingatie sheria na wajibu wake kwa kuvua samaki na dagaa kwa nyavu zinazostahili. 

"Kila mvuvi azingatie sheria zinazomuongoza katika utekelezaji wa majukumu yake, sisi kama halmashauri, tutaendelea kudhibiti uvuvi haramu ambao unaondoa na kuua masalia ya samaki kwa kiwango kikubwa, jambo ambalo litatukosesha mapato na wananchi kukosa samaki bora" Alisema Mbua

​Katika ripoti yake ya utekelezaji, Katibu wa mwalo wa Gana, Bwana Charles Gunda, amebainisha kuwa zana zilizoteketezwa zinajumuisha timba pisi 1627 na nyavu za makira inchi 3 pisi 80.

Kwa upande wake​Diwani wa Kata ya Ilangala, Mhe. Petro Majura, ametoa onyo kali kwa yeyote atakayeendelea kujihusisha na uvuvi haramu kuwa mkono wa sheria hautasita kuchukua mkondo wake.

​Mkuu wa Idara ya Kilimo, Mifugo, na Uvuvi, Ndg. Godfrey Ayako, amethibitisha kuwa serikali imejipanga kutatua changamoto ya upimaji wa mizigo ya dagaa ili kukuza sekta ya uvuvi.

​Cde. Ngubiagai amewahimiza wananchi kuchangamkia fursa za kiuchumi kwa kusajili vikundi vyao ili kufaidika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri.

​Mikopo hii ni kielelezo cha juhudi za dhati za viongozi hao katika kuinua uchumi wa vijana, wanawake, na watu wenye ulemavu ndani ya wilaya ya Ukerewe.

​Kwa hatua hizi za kishujaa, Cde. Ngubiagai na Ndg. Mbua wanaendelea kuweka misingi imara ya maendeleo endelevu na ulinzi wa rasilimali za ziwa kwa manufaa ya Watanzania wote.

No comments:

Post a Comment