Na: Mwandishi Wetu, Dodoma.
Leo Jumamosi, Septemba 21, 2024, ifikapo saa 05:59 usiku, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) inatarajia kufunga zoezi la kufanya masahihisho ya maombi ya mikopo yenye mapungufu na kasoro kadhaa.
Bodi ya Mikopo ilifungua dirisha la kufanya masahihisho kwa muda wa siku saba kuanzia Tarehe 15 Septemba, 2024 hadi leo Jumamosi, Septemba 21, 2024, ambapo zoezi hilo linafungwa rasmi.
Baada ya Bodi ya Mikopo kufunga zoezi la uombaji mikopo Septemba 14, 2024, ilibainika baadhi ya maombi yana kasoro na hivyo yanahitajika kufanyiwa masahihisho, ndiyo maana Septemba 15, 2024 bodi ilitoa siku saba za kufanya masahihisho ili maombi hayo yaweze kukamilika na hivyo yafanyiwe kazi.
Hivyo basi, ni muhimu kwa waombaji wote wa mikopo kuingia kwenye akaunti zao ili kuhakiki taarifa zao na endapo watabaini kuna mapungufu, basi watumie siku ya leo kufanya masahihisho ili maombi yao yaweze kufanyiwa kazi na endapo wamekidhi vigezo, wasikose fursa ya kupata mikopo ambayo ni muhimu katika safari ya masomo yao vyuoni.
Ikumbukwe kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/2025, serikali imetenga shilingi bilioni 787, kugharamia mikopo ya wanafunzi wapatao 250,000.
No comments:
Post a Comment