Na. Mwandishi Wetu
“Nimekuja kujifunza na kuhimiza masuala ya uadilifu, uzalendo na namna bora ya kutoa huduma kwa umma, kwa kuwa watumishi wa mamlaka hii wanawajibu wa kusanifu, kujenga na kusimamia mifumo ya TEHAMA Serikalini ili Serikali iweze kutoa huduma kwa umma kwa urahisi, haraka na gharama nafuu”.
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu Septemba 5, 2024 jijini Dodoma wakati alipotembelea ofisi za Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) lengo la kujifunza namna taasisi hiyo inavyofanya kazi na kuhimiza uwajibikaji kwa watumishi hao.
Mhe. Sangu alieleza kuwa Mamlaka ya Serikali ni muhimu sana kwa ustawi wa taifa, hivyo watumishi wake hawanabudi kuzingatia misingi ya uadilifu na uzalendo kwa kuwa taarifa nyingi za Serikali zinapita katika mifumo waliyoijenga na wanayoisimamia.
Aidha, aliongeza kwa kutoa pongezi kwa watumishi wa eGA kwa kuifanya Serikali kuwa ya kidijitali na kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma, mathalani mifumo iliyosanifiwa na kujengwa na eGA imeondoa upendeleo katika ajira za Serikali, wananchi wanaweza kulipia na kupata huduma mbalimbali wakiwa mahali popote na kwa wakati wowote.
Pia, alisisitiza watumishi wa Mamlaka hiyo kuendelea kuhimiza taasisi za umma kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa lengo la kuimarisha usalama wa mifumo ya Serikali na ya sekta binafsi iliyounganishwa na Serikali.
Awali, Katibu Mkuu-IKULU Bw. Mululi Majula Mahendeka alisema kuwa watumishi wa eGA wanatakiwa kufanyakazi kwa weledi na uadilifu ili kuifanya mifumo ya Serikali kuwa imara na inayoaminika kwa wananchi.
Vilevile, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Eng. Benedict Ndomba alisema kuwa pamoja na mambo mengine mamlaka imeshirikiana na taasisi husika kujenga Mfumo wa kielektroni wa Usimamizi wa Vyama vya Ushiriki (MUVU) ambao unarahisisha ukaguzi, usimamizi na uendeshaji wa Vyama vya Ushirika ili kuboresha utendajikazi, kuchochea mabadiliko ya kiuchumi na kuongeza uwazi na uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment