"WANANCHI WAUNGANISHIWE MAJI NDANI YA SIKU SABA" - WAZIRI AWESO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, September 5, 2024

"WANANCHI WAUNGANISHIWE MAJI NDANI YA SIKU SABA" - WAZIRI AWESO



Na Okuly Julius, Dodoma


Waziri wa Maji Jumaa Aweso amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazngira Dodoma (DUWASA), Mhandisi Aron Joseph kuhakikisha wananchi wote walioomba kuunganishiwa huduma ya maji waunganishiwe ndani ya siku saba tangu siku ya Maombi.

Aweso ametoa kauli hiyo leo Septemba 5,2024, jijini Dodoma wakati akizungumza katika kikao kazi kati ya DUWASA na viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kilicholenga kujadili masuala ya huduma za maji katika jiji la Dodoma.

"Akitokea mwananchi ameshakamilisha taratibu zote za kuunganishiwa maji basi aunganishiwe haraka na sio zaidi ya siku saba na Mwananchi anapotoa malalamiko yake yafanyiwe kazi haraka bila kujali hali yake maana kuna watu wengine mpaka wapigiwe simu na viongozi ndio wanafanya haraka, fanyeni hivyo hata kwa wananchi wa kawaida, " ameeleza Aweso

Pia amepiga marufuku tabia ya baadhi ya Watendaji wasio Waaminifu ya kuwabambikia wananchi bili za maji, ambapo Waziri Aweso amesema tabia hiyo inasababisha malalamiko kwa wananchi jambo ambalo sio malengo ya Serikali.

Katika hatua nyingine Aweso amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fedha nyingi kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji Dodoma Ili kukabiliana na uhaba uliopo Sasa kutokana na kuongezeka kwa idadi ya watu inayosababishwa na Serikali kuhamia Dodoma .

Amesema katika hatua za awali Serikali imetoa sh.bilioni 18 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya muda mfupi ambayo inaendelea kutekelezwa katika maeneo mbalimbali.

"Rais Dkt. Samia anatambua kuwa Dodoma bado kuna uhaba wa maji anaendelea na mikakati ya kuhakikisha wananchi wanapata maji kwa kutoa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maji,"amesema Aweso

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe Rosemary Senyamule amewataka viongozi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, kuhakikisha wanalinda vyanzo vya maji na kuwaelimisha wananchi madhara ya kuchoma moto katika maeneo yenye miundombinu ya maji.

"Kuna watu bado kule Mzakwe wanachoma moto karibu na kile chanzo ambacho ndio kikubwa kwa Dodoma na ndicho kinachohudumia eneo kubwa la Mji wetu, sasa wanafanya hivyo na viongozi mnawaangalia tu hata hamchukui hatua zozote ndio maana wale wananchi wanaendelea kufanya uharibifu, " ameeleza Senyamule

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA Mhandisi Aron Joseph amesema Mamlaka hiyo imechukua maoni yote yaliyotolewa na viongozi hao wa Serikali za Mitaa, na kuahidi kuyajibu kwa njia ya maandishi na kuwapatia kila mmoja nakala itakayokuwa na Majibu yote.

Moja ya suala ambalo Viongozi hao wameshauri ni namna ya kushirikiana kisheria na DUWASA katika ulinzi wa miundombinu ya maji, ambapo Mhandisi Aron amesema kuwa wataanza kutoa Shilingi Laki moja kwa wananchi watakaotoa taarifa sahihi za waharibifu na wanaojiunganishia maji kinyume na utaratibu.



No comments:

Post a Comment