Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi akisisitiza jambo katika Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam lililobebwa na kauli mbiu isemayo “Kuwainua Vijana katika safari yao ya Taaluma na Biashara”.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB), Eng. Bernard Kavishe, akitoa maelezo kuhusu Jukwaa la Wahandisi Vijana, jijini Dar es Salaam lililobebwa na kauli mbiu isemayo “Kuwainua Vijana katika safari yao ya Taaluma na Biashara”.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi (Watatu kushoto) pamoja na viongozi wengine wa Serikali, akipata maelezo kutoka kwa mtaalam wa chuo cha St. Joseph alipotembelea banda la Chuo hicho katika Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam.
Wadau mbalimbali wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi (hayupo pichani) katika Jukwaa la Wahandisi Vijana lililofanyika jijini Dar es Salaam
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi akimpa cheti mmoja wa wanafunzi waliofanya vizuri katika Tasnia ya Uhandisi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini mara baada ya kufungua Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam.
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Patrobas Katambi (katikati), Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhandisi, Zena Said (Watatu kulia), Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, (Watatu Kushoto) na Viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kufungua Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi Wetu Dar es Salaam
Serikali imesema kuwa imeandaa mkakati maalum wa kutoa fursa za ajira na kutengeneza mazingira wezeshi kwa wahandisi wazawa kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo nchini ili kuwainua kichumi na kuleta maendeleo nchini.
Ameyasema hayo, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mheshimiwa Patrobas Katambi leo, Septemba 3, 2024 wakati akifungua Jukwaa la Wahandisi Vijana jijini Dar es Salaam lililobebwa na kauli mbiu isemayo “Kuwainua Vijana katika safari yao ya Taaluma na Biashara” ambalo limeratibiwa na Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB).
“Serikali imeanzisha Sera ya maendeleo ya Vijana, lengo lake ni kutatua changamoto za ajira kwa vijana katika maeneo ya ukuzaji wa taaluma, ujuzi, ubunifu na uvumbuzi, pia Sera hii itaangazia namna ya kuinua wazawa katika maeneo mbalimbali” amesema Katambi.
Amefafanua kuwa kupitia Sera hiyo wataalamu mbalimbali ikiwemo wahandisi watanufaika kwa kuweza kupata nafasi ya kutekeleza miradi ambayo walikuwa wakishindwa kutekeleza awali kutokana na changamoto za kisera na sheria.
Kadhalika, ameongeza kuwa katika kuhakikisha Serikali inalinda soko lake la ndani pia inadhibiti uagizwaji wa vifaa vya ujenzi kutoka nje ya nchi ambavyo vinaweza kupatikana nchini.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde amesema kuwa Wizara itaendelea kuunga mkono jitihada zinzofanywa na ERB za kuinua Wahandisi ili kuwawezesha kutekeleza miradi mikubwa nchini.
“Niwapongeze kwa kuanzisha jambo hili ambalo litaota, kumea, kukua na kuleta maendeleo kupitia wahandisi hawa, niwahakikishie kuwa Wizara inaandaa mpango kabambe wa kuongea na wadau kuhakikisha fedha nyingi zinapatikana ili kuwasaidia wahandisi kuanzisha Kampuni zao”, ameeleza Dkt. Msonde.
Aidha, Dkt. Msonde amewataka Wahandisi hao kutumia Jukwaa hilo vizuri ili kuweza kuleta matokeo chanya na hatimaye kuboresha maisha yao na uchumi wa Taifa kwa ujumla kupitia tasnia ya Uhandisi.
Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi, Mhandisi, Mwanasheria Menye Manga amesema kuwa Jukwaa hilo ambalo limeanza mwaka huu linatoa fursa kwa vijana hao kupata ujuzi, uzoefu na maoni kutoka kwa wadau wa Taaluma ya Uhandisi ndani na nje ya nchi.
Ameongeza kuwa jumla ya Wahandisi 24 wamekula kiapo katika Kongamano hilo, na Wanafunzi 15 kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini waliofanya vizuri katika masomo ya uhandisi wamepewa vyeti.
Awali akitoa maelezo ya Kongamano hilo, Msajili wa ERB, Mhandisi Bernard Kavishe amesema kuwa Kongamano hilo linaenda sambamba na Siku ya Wahandisi pamoja na mbio za riadha maalum kwa ajili ya kuchangisha fedha za kusaidia programu ya kufadhili walimu wa kujitolea wa masomo ya Sayansi na Hisabati kwa Shule za Sekondari.
Kongamano hili la siku mbili limehudhuriwa na wadau mbalimbali ikiwemo wahandisi mbalimbali kutoka ndani ya nchi na nchi jirani za Kenya, Ethiopia na Sudan Kusini, wadau mbalimbali pamoja na wanafunzi waliofanya vizuri katika masomo yao ya kihandisi kutoka Vyuo Vikuu mbalimbali nchini.
No comments:
Post a Comment