Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe Dkt Dotto Biteko amesema Serikali haitapuuza wala kudogosha Mchango unaotolewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali NGOs
Amesema Mashirika hayo yamefanya kazi kubwa ikiwemo kuwapa ajira vijana wa Kitanzania ambao wangepaswa kuajiriwa na Serikali jambo ambalo lingekuwa gumu kwa Serikali kuwaajiri wote.
Dkt.Biteko ametoa kauli hiyo leo Septemba 6,2024 wakati wa Kilele cha Jukwaa la Mwaka la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 2024, iliyoanza Septemba 4 jijini Dodoma, inayokwenda na kauli mbiu ya Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ni Wadau Muhimu, Washirikishwe Kuimarisha Utawala Bora.
"Serikali ni rafiki wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa sababu wamesaidia sana kuleta utulivu nchini kwani imesaidia kupunguza umasikini kwa vijana wengi wa kitanzania kwa kuwapatia ajira,"
Na kuongeza kuwa“Serikali kupitia Wizara ya Fedha ipo katika mchakato wa kuaanda mwongozo wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ambao ukikamilika, bajeti ya Mashirika hayo itakua inajumuishwa kwenye bajeti kuu hivyo basi, natoa wito kwenu kuwa mkawahudumie Watanzania kwa upendo katika sekta zote na mkawe waaminifu kwenye fedha zinazotolewa kwa ajili ya kurahisisha maisha ya Watanzania,” amesema Dkt. Biteko.
Dkt. Biteko ametoa rai kwa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kuhamasisha ajenda ya matumizi ya Nishati Safi kwa wananchi ili itapofika 2034 asilima 80 wawe wanaweza kutumia nishati safi na kuondokana na magonjwa yanawakumbuka wengi kwa kutumia nishati zinazowaathiri.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema, kupitia uchambuzi wa taarifa za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali 1,368, imebainika kuwa jumla ya Shilingi 2.6 trilioni zilipokelewa na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na kwamba kiasi cha Shilingi trilioni 2.4 kilitumika kwa ajili ya utekelezaji wa miradi katika nyanja mbalimbali.
“Sekta iliyoongoza kwa mwaka 2023 ilikuwa ni Sekta ya Afya, ikifuatiwa na Uwezeshaji wa Jamii Kiuchumi na Ulinzi wa Jamii. Sekta nyingine ni pamoja na Uhifadhi wa Mazingira, Sekta ya Elimu, Sekta ya Kilimo, Utawala Bora, Sekta ya Maji, Masuala ya Jinsia na Haki za Binadamu. Makundi yaliyonufaika zaidi na miradi hiyo ni wanawake ambao walifikiwa kwa takribani asilimia 47.4 na vijana ambao walifikiwa kwa takribani asilimia 30.5,” amesema Dkt. Gwajima.
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mashirika Yasiyo Ya Kiserikali Jasper Makala ameishukuru Serikali kwa juhudi inazofanya za kuwawekea mazingira wezeshi katika utekelezaji wao wa majukumu.
“Mashirika Yasiyo ya Kiserikali yanatambua kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Awamu ya
Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan na pasina shaka kuwa Serikali yetu inayatambua na kuyathamini Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwani kwa miaka minne mfululizo tumepata Viongozi wa Juu wakuu wa Nchi kutusikiliza na kuzungumza nasi,” amesema Makala.
No comments:
Post a Comment