Na Lusungu Helela- Tabora
Serikali imesema haitawavumilia Watumishi wa Umma wenye kasumba ya kufanya kazi kwa mazoea hali inayopelekea malalamiko kutoka kwa wananchi kwa kushindwa kupata huduma bora
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Deus Sangu ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza kwenye Kikao kazi cha Watumishi wa Manispaa ya Tabora mara baada kusikiliza changamoto zinazowakabili na kuzitafutia ufumbuzi, ikiwa ni ziara ya kimkakati ya kuwafuata watumishi katika maeneo yao ya kazi badala ya kuja Dodoma
Amesema tabia hiyo imekuwa ikikwamisha azma ya Rais Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan ya kuona Wananchi wanahudumiwa ipasavyo katika ofisi za Serikali
Amewataka Watumishi hao kutambua kuwa suala la kutoa huduma bora kwa wananchi si hisani bali ni wajibu
Katika hatua nyingine Mhe. Sangu amezitaka Mamlaka za ajira na nidhamu kusimamia haki na stahiki zote za watumishi huku akizionya Mamlaka hizo kushauri ipasavyo bila kuwaumiza watumishi kwa lengo la kuwafurahisha Viongozi wao.
Amesema ni jambo la aibu kuona Watumishi wakiwasilisha changamoto zao mbele ya Viongozi wa Kitaifa wanapofanya ziara katika maeneo yao ilhali changamoto hizo zingetafutiwa ufumbuzi katika ngazi ya Wilaya au Mkoa
Amesema kitendo hicho kinaonesha kuwa baadhi ya Watumishi hawawajibiki ipasavyo katika kutekeleza majukumu yao.
" Haipendezi kuona Watumishi wakiwa hawatimizi wajibu wao wakitumia simu na kupiga soga muda wote kipindi cha muda wa kazi " amesema Mhe.Sangu
Sambamba na hilo Mhe.Sangu ametoa rai kwa Watumishi kujiepusha kutenda vitendo vitakavyopelekea kufukuzwa kazi huku akisisitiza kuwa mchakato kurudishwa kwenye utumishi wa umma ni jambo gumu
Hivyo, Mhe.Sangu amewasihi Watumishi wa Umma nchini kujiepusha vitendo hivyo kwani mchakato wake wa kupata kibali cha kurudishwa unachukua muda mrefu
No comments:
Post a Comment