SITOSITA KUMCHUKULIA HATUA ATAKAEJIUSISHA NA UBADHIRIFU WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 - Mhe. Mchengerwa - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, September 21, 2024

SITOSITA KUMCHUKULIA HATUA ATAKAEJIUSISHA NA UBADHIRIFU WA MIKOPO YA ASILIMIA 10 - Mhe. Mchengerwa


Na. James K. Mwanamyoto, OR-TAMISEMI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema hatosita kuwachukulia hatua za kinidhamu na kisheria maafisa maendeleo ya jamii, wasimamizi wa fedha, waratibu wa mikopo, wahasibu na maafisa TEHAMA wa Mikoa na Wilayq ambao watabainika kujihusisha na ubadhirifu wa fedha za mikopo ya asilimia 10 zinazotolewa na Halmashauri kwa vikundi vya wanawake,vijana na watu wanye ulemavu.

Waziri Mchengerwa ameyasema hayo leo Jijini Dodoma katika ukumbi wa Chuo cha Mipango, wakati akifunga mafunzo ya wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini.
“Mikopo hii inatolewa na Serikali kwa ajili ya kuwawezesha kiuchumi wanaweke, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujikomboa kiuchumi kwa kufanya shughuli mbalimbali za ujasiriamali, hivyo sitosita kuwachukulia hatua watakaokwamisha makundi lengwa kupata mikopo,” Mhe Mchengerwa amesisitiza.


Mhe. Mchengerwa amesema mikopo hii ikisimamiwa vizuri na kuwafikia walengwa itabadilisha maisha ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo waende kutoa elimu ya namna bora ya kuitumia mikopo hiyo kuboresha maisha yao ili waweze kufanya marejesho kwa wakati na kuwezesha wengine kunufaika.

Waziri Mchengerwa amewataka wasimamizi wa mikopo ya asilimia 10 kuratibu utoaji wa mikopo hiyo kwa uzalendo ili iwanufaishe walengwa na iwe na tija kwa jamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla kama ilivyo kusudiwa na Serikali.

Mpaka kufika mwaka wa fedha 2024/25 fedha ambazo zimetengwa kutoka kwenye marejesho ya mikopo ya nyuma pamoja na mapato ya ndani ya Halmashauri tangu utoaji wa mikopo hii ulipositoshwa ni zaidi ya shilingi bilioni 160 kwa Halmashauri zote nchini na fedha hizi zitatumika kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, pamoja na usimamizi wa mikopo hiyo.

Ikumbukwe kuwa mikopo hii inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote nchini.

No comments:

Post a Comment