DC KAGANDA ATATUA MGOGORO KATI YA MUWEKEZAJI NA HIFADHI YA TAIFA YA ZIWA MANYARA - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, March 14, 2026

DC KAGANDA ATATUA MGOGORO KATI YA MUWEKEZAJI NA HIFADHI YA TAIFA YA ZIWA MANYARA


Mkuu wa Wilaya ya Babati, Mhe. Emmanoela Kaganda, ametembelea na kukagua eneo lenye mgogoro kati ya muwekezaji na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara katika Kijiji cha Moya Mayoka, Kata ya Magara.

Akizungumza na wananchi wa kijiji hicho, DC Kaganda amebainisha kuwa mipaka kati ya Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara na Kijiji cha Moya Mayoka vemezingatia alama za mipaka (bikoni) zilizowekwa katika eneo la hifadhi ili kuzuia muingilio na maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uhifadhi na mwekezaji.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuacha tabia ya kuingia ndani ya hifadhi na kufanya shughuli nyingine ambazo zitaathiri uoto wa asili, huku akisisitiza kuwa vitendo vya kujichukulia maeneo kiholela vilivyokuwa vikifanyika miaka ya nyuma haviruhusiwi hata kidogo.

Aidha DC Kaganda aliwataka viongozi wa Halmashauri ya Kijiji, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri, Kamishna wa Ardhi pamoja na uongozi wa Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara kushirikiana kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kulinda uhifadhi.

Vilevile amesisitiza umuhimu wa kupima ardhi ya kijiji hicho ili kipate cheti na hati ya kijiji, hatua itakayosaidia kuondoa migogoro ya ardhi kati ya kijiji na hifadhi.

Sambamba na hayo akawapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa juhudi zao za kutunza mazingira yanayozunguka eneo lao.

Kwa upande wa Diwani wa Kata ya Magara pamoja na wananchi wa Kijiji cha Moya Mayoka walimpongeza Mkuu wa Wilaya kwa kutoa elimu ambayo imewafungua katika masuala ya uhifadhi na kulinda hifadhi za taifa huku wakisisitiza kuwa itasaidia kutatua na kuzuia kabisa migogoro kati ya wananchi na Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.

No comments:

Post a Comment