Na. Elimu ya Afya kwa Umma.
Kikao Kazi cha Kuandaa Mpango wa Kuharakisha Utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii nchini kimeendelea Jijini Dar Es Salaam huku maoni mbalimbali yakitolewa ikiwemo nyenzo zitakazotumika ili kufanikisha shughuli zao za kila siku ikiwemo umuhimu wa matumizi ya teknolojia ikiwemo teknolojia ya mwasiliano kama vile vipaza sauti(Megaphones).
Miongoni mwa matumizi hayo ya nyenzo hizo muhimu ni pamoja na umuhimu wa matumizi ya vishikwambi ambapo baadhi ya Washiriki wa Mkutano huo wameshauri Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kuunganishwa na vyuo vya teknolojia ikiwemo Chuo cha Sayansi na Teknolojia Dar es Salaam (DIT) ili waweze kujifunza matumizi sahihi ya Teknolojia mbalimbali katika utendaji wa shughuli zao.
Aidha, katika Kikao hicho,suala la kujumuishwa kwenye bima ya Afya kwa wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii limejadiliwa ambapo baadhi ya washiriki wamesema kuna umuhimu mkubwa wa kufanya jambo hilo.
Halikadhalika, suala la uimarishaji wa miundombinu ya usafiri hasa katika kutumia Mfumo wa M-mama , pamoja na malipo kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii vimejadiliwa katika kikao hicho .
Kikao hicho kimehudhuriwa na Viongozi na Wataalamu wa Afya kutoka Wizara mtambuka ikiwemo Wizara ya Afya, Ofisi ya Rais TAMISEMI akiwemo Dkt.Ona Machangu, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Dkt.May Alexander Mratibu wa Afya Ngazi ya Jamii, Ofisi ya Rais TAMISEMI,Maafisa wengine mbalimbali na wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali.
Kikao hicho kimekutanisha Wadau wa sekta ya Afya kutoka Tanzania Bara na Tanzania Visiwani kwa kushirikiana na Shirika la Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa la Afrika (Africa CDC) pamoja na Wadau wengine huku lengo ni kujadili masuala ya Uratibu kwa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii na kupendekeza utaratibu ambapo wadau wanaotekeleza afua zinazohusiana na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wataweka Mipango ya Utekelezaji.
No comments:
Post a Comment