🎈🎈Asema wananchi wana wajibu wa kufuatilia utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yao
🎈🎈Aeleza umuhimu wa Sensa ya Watu na Makazi katika kuleta maendeleo
Naibu Waziri wa Nishati na Mbunge wa Viti Maalum Vijana Taifa, Mhe. Judith Kapinga amesema dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wanashirikishwa katika kufanya maamuzi ya maendeleo katika maeneo yao.
Aidha, Viongozi katika ngazi mbalimbali wahakikishe maamuzi hayo yanazingatia mipango na programu zinazoakisi hali halisi ya wananchi, mahitaji yao pamoja na vipaumbele.
Mhe. Kapinga amesema hayo leo Septemba 30, 2024 wakati akifungua Mafunzo ya Matumizi ya Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa Viongozi, Watendaji na Wadau wa Wilaya ya Mbinga.
Ameongeza kuwa, Serikali inataka kuona wananchi wanasimamia maendeleo yao kwa kufanya maamuzi na kuweza kufuatilia na kusimamia utekelezaji wake kwa kutumia vigezo vya kitakwimu.
Amesema Sensa za Watu na Makazi hufanyika kwa lengo la kupata takwimu za msingi za watu na hali ya makazi yao ili kusaidia kutunga Sera, kupanga na kufuatilia mipango ya maendeleo ya kimkakati inayolenga kukuza uchumi wa nchi na watu wake.
"Kupitia mafunzo haya tutaweza kuona hali halisi ya Halmashauri yetu, kwa kulinganisha na baadhi ya viashiria vya ngazi ya Taifa na hata Halmashauri nyingine katika kujiletea maendeleo ya Mkoa wetu wa Ruvuma.' Amesema Kapinga
Amesisitiza kuwa, matokeo ya Sensa ya mwaka 2022 yanalenga kuisaidia Serikali na wadau kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa mipango na programu za maendeleo ya kitaifa, kikanda na kimataifa kwa lengo la kukuza uchumi na kuondoa umaskini.
Ameongeza kuwa, matokeo hayo ya Sensa pamoja na takwimu nyingine ndio dira katika kufanya maamuzi ya msingi yanayohusu uanzishwaji wa miradi mipya, uimarishaji na uboreshaji wa utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi zikiwemo za kijamii kama elimu, afya, maji pamoja na huduma nyingine kama za kiuchumi na miundombinu.
No comments:
Post a Comment