Wadau wa Utalii wametakiwa kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kulinda maliasili na tamaduni zilizopo nchini Tanzania ili kuwa na biashara ya utalii endelevu lakini pia wametakiwa kubuni mbinu mpya za kutangaza na kuendeleza biashara ya utalii nchini.
Rai hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula (Mb) wakati wa maadhimisho ya siku ya Utalii Duniani Jijini Arusha ambayo yameandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Rethinking Tourism Africa kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).
Mhe. Kitandula katika hotuba yake alipongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kutangaza utalii kupitia filamu za Tanzania The Royal Tour na Amazing Tanzania kwa kuwa zimekuwa kichecheo kikubwa kwa wageni kuja kutembelea vivutio vya utalii nchini.
Kupitia filamu ya Tanzania The Royal Tour, imepelekea idadi ya watalii kuongeza kufikia milioni moja na laki nane kwa takwimu za Januari 2024 zinazotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikiwa masuala ya Utalii (UNWTO) idadi ambayo imevunja rekodi kwa 24% ukilinaganisha na idadi ya kipindi kama hicho mwaka 2023.
Mhe. Kitandula alisema kwamba kauli mbiu ya siku ya utalii mwaka ambayo ni “Utalii na Amani” ni kielelezo na kiunganishi kikubwa kwa kuwa biashara ya utalii inaunganisha jamii mbalimbali kwa urahisi, utalii unaleta maelewano kwenye jamii lakini pia inafanya Dunia kuwa sehemu salama.
Vilevile Mhe. Kitandula alitumia fursa hiyo ya kuwakaribisha wadau kuwekeza kwenye biashara ya utalii kwa vile Tanzania ina utajili mkubwa wa maliasili ambao unapatikana Tanzania Bara na Zanzibar, pia aliongeza kuwa kumekuwepo na ongezeko kubwa la watalii hivyo kufanya mahitaji ya malazi kuongezeka.
“Nitumie fursa hii kuwakaribisha wawekezaji wa huduma za malazi kuja kuwekeza kwa wingi ili tuweze kuziba upungufu uliopo kwa sasa” alisema Mhe. Kitandula.
Akimkaribisha Mhe. Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mkuu wa chuo Cha Uhasibu, Prof. Eliamani Sedoyeka aliipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa juhudi kubwa inazoweka za kuhakikisha biashara ya utalii inakuwa endelevu kwa manufaa ya taifa.
Maadhimisho wa Siku ya Utalii Duniani yamehudhuriwa na Waziri wa Habari , Utamaduni na Utalii kutoka Jimbo la Jubaland Nchini Somalia Mhe. Abdifatah Mohamed Muktar, mwakilishi kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa linashughulikia Utalii(UNWTO) Dkt. Marcel Leijzer, na baadhi ya watumishi wanaoshughulika na masuala ya Utalii kwenye taasisi za serikali na binafsi.
No comments:
Post a Comment