Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amemuelekeza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde kuusimamia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kushirikiana na Halmashauri, Manispaa, Miji na Majiji katika ujenzi wa nyumba za kisasa za Watumishi wa umma zenye gharama nafuu.
Bashungwa ametoa agizo hilo Mkoani Pwani mara baada ya kufungua nyumba sita za Wakuu wa Idara na Vitengo zilizojengwa na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kwa lengo la kutatua changamoto za makazi bora kwa Watumishi.
“Namuelekeza Naibu Katibu Mkuu Dkt. Msonde afike mara moja Chalinze na kuangalia mfano wa nyumba hizi, kuona namna TBA watakavyojipanga kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze pamoja na Halmashuri zote nchini katika kuboresha makazi ya Watumishi”, amesema Bashungwa.
Bashungwa ameielekeza TBA kuendelea kuwa wabunifu kwa kutafuta teknolojia ambayo itatumika katika ujenzi nyumba za gharama nafuu na makazi bora kwa Watumishi wa umma.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa ni maelekezo ya Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa Taasisi kupunguza utegemezi wa fedha za Serikali kwa kuingia ubia na sekta binafsi ambapo tayari Wizara ya Ujenzi kupitia TBA imerekebisha sheria itakayoiwezesha kushirikiana na Sekta Binafsi katika ujenzi wa majengo na nyumba za makazi.
Bashungwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze kwa ujenzi wa nyumba bora za Watumishi ambazo zimeweka mazingira wezeshi na kutoa wito kwa Watumishi hao kuendelea kutoa huduma bora kwa Wananchi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Shaibu Ndemanga amesema kuwa katika mwaka wa fedha 2022/23 Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 800 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba sita na mwaka wa fedha 2023/24 Halmashauri ilipokea kiasi cha Shilingi Milioni 320 kwa ajili ya ujenzi wa nyumba mbili za Wakuu wa Idara katika Kitongoji cha Kibiki.
Akitoa taarifa ya mradi, Mkuu wa Kitengo cha Miundombinu, Eng. Olais Sikoi ameeleza kuwa ujenzi wa nyumba sita za Wakuu wa Idara na Vitengo umetekelezwa kwa njia ya “Force Account” na umekamilika kwa asilimia 98 ambapo kazi zilizobakia ni pamoja na uwekaji wa vioo kwenye milango katika nyumba 5, kuunganisha mfumo wa maji safi na kuunganisha umeme.
No comments:
Post a Comment