Dkt. Mpango atoa wito kwa Watanzania kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 10, 2024

Dkt. Mpango atoa wito kwa Watanzania kujiandikisha kwa ajili ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa


Na OR TAMISEMI, Tabora


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Isidor Mpango ametoa wito kwa watanzania kwenda kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura ili kuwachagua viongozi wa Serikali za Mitaa wanaowataka.

Dkt. Mpango alitoa kauli alipokuwa akiongea na wananchi wa Manispaa ya Tabora tarehe 9 Oktoba, 2024 na kuwataka wananchi kote nchini wenye sifa kwenda kujiandikisha katika daftari la Wapiga Kura kuanzia tarehe 11 Oktoba, 2024 hadi tarehe 20 Oktoba, 2024 kote nchini na kusisitiza kuwa njia pekee ya kuwachagua Viongozi waadilifu au kuwaondoa Viongozi wabaya ni kupiga kura katika uchaguzi huo utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

Dkt. Mpango pia amewataka wanawake kwenda kuchukua fomu ili kugombea nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024 kwani wanawake wanaweza kuleta maendeleo nchini kama anavyofanya jemedari Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwaunganisha wananchi na kuwaletea maendeleo kwenye Sekta zote.

Aidha, aliwaagiza Viongozi wa Chama na Serikali kwenda kuwatembelea wananchi vijijini ili kujionea changamoto zao na kuzifanyia kazi badala ya kusubiri kipindi cha uchaguzi wanapokwenda kuwaomba kuwapigia kura.

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Dkt. Mpango alipokea ombi la kuifanya Manispaa ya Tabora kuwa Jiji na ndipo aliiagiza Ofisi ya Rais TAMISEMI kufanya tathmini na kujiridhisha kama vigezo vya Manispaa ya Tabora kuwa Jiji vinafikiwa.

“napenda kutumia nafasi hii kuielekeza Ofisi ya Rais TAMISEMI kuanza kufanya tathmini ili ijiridhishe na masharti na vigezo vinavyotakiwa ili kuweza kupata hadhi ya kuwa Jiji” alisema Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango

Katika uwanja wa Chipukizi alipotoa hotuba Mheshimiwa Dkt. Mpango yanafanyika maadhimisho ya juma la Elimu ya Watu Wazima ambayo yanafanyika Kitaifa mkoani Tabora na yalianza tangu tarehe 7 Oktoba, 2024 na yatafikia kilele tarehe 11 Oktoba, 2024 yenye kauli mbiu “Ujumuishi katika Elimu bila ukomo kwa ujuzi, ustahimilivu, amani na maendeleo”

No comments:

Post a Comment