“Msitoke Mafia mpaka Kivuko kianze kutoa huduma kwa Wananchi”
Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amempgia simu na kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi Eng. Aisha Amour na Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Ufundi na Umeme (TEMESA), Lazaro Kilahala kufika mara moja katika Kisiwa cha Mafia kupiga kambi kusimamia matengenezo ya Kivuko cha MV Kilindoni na kuhakikisha hawatoki mpaka huduma ya usafiri wa kivuko kati ya Nyamisati - Mafia itakaporejea na kutoa huduma kwa wananchi.
Bashungwa ametoa maelekezo hayo wakati akitoa ufafanuzi kwa Wananchi kuhusu kusimama na kukosekana kwa huduma ya usafiri wa vivuko katika Wilaya ya Mafia Mkoani Pwani ambapo Wananchi wamelalamikia kukosa huduma ya vivuko na kupelekea kutumia vyombo vya usafiri visivyo salama na uhakika pamoja na kushindwa kusafirisha bidhaa na huduma nyingine.
“Katibu Mkuu kufika kesho kutwa wewe au Naibu Katibu Mkuu uje hapa Mafia uambatane na Mtendaji Mkuu wa TEMESA mpige kambi muone kilio na uchungu wa wananchi wa Mafia wanaoupata, Msitoke hapa mpaka kivuko kianze kutoa huduma kwa wananchi. Kivuko kikianza kufanya kazi ndio mnipigie simu niweze kuwaruhusu kutoka huku Mafia”, amesisitiza Bashungwa.
Waziri Bashungwa ameeleza kuwa Serikali inatambua usafiri unaotumika kufika katika kisiwa cha Mafia ni usafiri wa vivuko na ndege ambapo sasa Serikali inaendelea na jitihada za kurejesha huduma ya usafiri wa vivuko kwa kuwa sio wananchi wote wana uwezo wa kutumia usafiri wa ndege.
Aidha, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa inaendelea na ukarabati wa Meli ya TNS Songosongo itayosaidia kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi wa Mafia wakati Kivuko cha MV Kilindoni kikiwa kwenye matengenezo.
Bashungwa ameeleza kuwa Serikali imetenga fedha zaidi ya Shilingi Bilioni 9 kwa ajili ya ujenzi wa kivuko kipya kitakachotoa huduma za usafiri kati ya Mafia na Nyamisati na hivyo kuongeza idadi ya vivuko kuwa vitatu.
Katika nyakati tofauti, Wananchi wa Kilindoni Wilayani Mafia wameiomba Serikali kusimamia na kutatua kero ya huduma ya usafiri wa vivuko wanayoipata katika Wilaya hiyo ambayo imesababisha kuongezeka kwa gharama za maisha na wananchi kushindwa kupata huduma nyingine za kijamii.
No comments:
Post a Comment