DUWASA YATAKIWA KUSAMBAZA MAJI ENEO LA KISASA CHINI YA WIKI NNE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Sunday, October 27, 2024

DUWASA YATAKIWA KUSAMBAZA MAJI ENEO LA KISASA CHINI YA WIKI NNE


Na Okuly Julius Dodoma


Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini Jabir Shekimweri ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) kukamilisha kwa muda usiozidi wiki nne zoezi la usambazaji wa maji ya kisima cha Kisasa Mwangaza.

Shekimweri ametoa maagizo hayo leo Oktoba 27,2024 jijini Dodoma, alipotembelea na kukagua maendeleo ya Mradi huo ambao unatekelezwa na DUWASA kupitia mapato yake ya ndani,
kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa huduma ya maji kwa wakazi wa eneo hilo.

"Nimesikia usambazaji wa maji kutoka katika kisima hichi utafanyika ndani ya Wiki nne, mimi kwangu naona ni nyingi kwa sababu eneo hili lina mtandao wa maji tayari changamoto ilikuwa ni upungufu wa maji niwaombe DUWASA unganisheni maji haya katika mtandao uliopo ili kuongeza upatikanaji wa maji na shughuli hiyo ifanyike chini ya Wiki nne, " amesisitiza Shekimweri

Pia shekimweri ameitaka DUWASA kuhakikisha wanatunza eneo hilo kwa kupanda miti maji na kuhakikisha panakuwa salama kwani eneo hilo linaweza kuwa chanzo kizuri cha maji na kusaidia kuondoa changamoto ya maji kwa wakazi wa Kisasa na maeneo ya jirani


Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Dodoma mjini, ambaye pia ni Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema zoezi la uchimbaji visima ndani ya jiji la Dodoma na maeneo ya pembezoni limekua na manufaa makubwa katika kuendelea kupunguza adha ya maji kwa kuzingatia Dodoma ni Mji ambao unakuwa kwa kasi hivyo mahitaji ya huduma ya maji yanaongezeka.

"DUWASA wanafanya kazi nzuri ya kuhakikisha huduma upatikanaji wa maji inaendelea kuimarika siku hadi siku kwani Dodoma kwa sasa inakuwa kwa kasi baada ya Serikali kuhamia," amesema Mavunde

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Dodoma mjini Charles Mamba ameeleza juu ya Suluhu ya changamoto ya upatikanaji wa maji katika jiji la Dodoma.

" kinachofanyika hapa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM hivyo DUWASA wanashiki kikamilifu katika utekelezaji wake, hivyo niwapongeze DUWASA kwa hichi wanachofanya ya kuhakikisha Dodoma inapata maji ya kutosha," amesema Mamba

No comments:

Post a Comment