Na Okuly Julius Dodoma
Katika muendelezo wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, Leo Oktoba 08, 2024, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA), iko "Mtaa kwa Mtaa" kuwasikiliza wananchi na wateja wa Mtaa wa Mlimwa C na Ubalozi wa Mbogoni wakiongozwa na Balozi wa CURTEUS MBOGONI, ambapo malalamiko yao ni kutopata maji na kuingiziwa bili ilihali hawapati huduma ya maji.
Akijibu Malalamiko hayo ya wateja, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja - DUWASA Bi. Lena Mwakisale amesema suala la kusomewa bili ya maji kwa wateja ni la kila mwezi na haki ya Mteja ni kushirikishwa wakati wa usomaji wa mita ya maji.
Bi. Lena amewaomba wananchi pindi wapatapo ujumbe wa bili wakasome kwenye mita zao ili kujua kama bili iliyotumwa ina uhalisia.
Pia amesema DUWASA inatambua changamoto hiyo ya Upungufu wa maji na wapo katika hatua nzuri ya kuhakikisha wananchi wa Mtaa wa Mlimwa C wanaunganishwa kwenye Bomba kubwa lililopo maeneo ya Wajenzi.
Elimu kwa wateja inaendelea kutolewa na DUWASA "Mtaa kwa Mtaa" ikiwashirikisha viongozi wa Serikali za Mitaa katika maeneo husika ili kujua changamoto zinazowakabili wateja wao na kuzitatua.
No comments:
Post a Comment