🎈🎈Yashiriki Samia Kilimo Biashara Expo 2024
🎈🎈Kugawa majiko 790 Wilaya ya Gairo
🎈🎈Yanatunza mazingira na rafiki kwa afya ya watumiaji
Imeelezwa kuwa, Majiko Banifu yanayotolewa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Maonesho ya Samia KILIMO Biashara Expo 2024 yanapatikana kwa gharama nafuu, yanatunza mazingira, yanadumu na rafiki kwa afya ya watumiaji.
Hayo yamebainishwa leo tarehe 6 Oktoba, 2024 na Mkuu wa wilaya ya Gairo, Mhe Jabir Makame wakati akizungumza na wananchi alipotembelea banda la REA yanapofanyika maonesho hayo kwa msimu wa tatu mwaka huu kijiji cha Leshata wilaya ya Gairo mkoani Morogoro.
Mhe. Makame ameeleza kuwa, majiko banifu ni rafiki na salama kwa afya ya watumiaji nchini na kuwasisitiza wananchi wake wayatumie kwa kuwa yanauzwa na kupatikana kwa bei rafiki.
Makame amesema wananchi hao wanakwenda kushuhudia mageuzi makubwa ya utunzaji wa mazingira kupitia Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ambao kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Amesema Gairo inatekeleza kampeni ya URITHI WA KIJANI yenye lengo la kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya tabianchi ambayo yana athari katika Sekta ya Kilimo na Mifugo.
Ametaja wadau wanaoshiriki kuwa ni pamoja na Mashirika ya Mazingira, Kampuni za Gesi, Kampuni zinazotengeneza mkaa mbadala ikiwemo STAMICO, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira pamoja na Wizara ya Nishati.
Naye, Mhandisi wa REA Deusdedith Malulu ameongeza kuwa, majiko hayo yanatunza mazingira kwa kutumia kiasi kidogo cha mkaa na ufanisi wake ni mkubwa.
"Majiko haya hayaruhusu hewa ya mkaa ambayo ni hatari kwa watumiaji kutoka nje kwa aina ya muundo wake na hivyo kuwa rafiki kwa mazingira" amesema Mha. Maluku
Mha. Malulu amesema kupitia maonesho hayo wananchi wa wilaya hiyo wameanza kupatiwa majiko banifu na REA imeaza kutoa majiko 790 ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ajenda ya matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.
No comments:
Post a Comment