SERIKALI YASISITIZA KUWEKA MAZINGIRA MAZURI KWA MAKANDARASI WANAWAKE - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 31, 2024

SERIKALI YASISITIZA KUWEKA MAZINGIRA MAZURI KWA MAKANDARASI WANAWAKE


Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour akizungumza wakati akifungua Kongamano la Nne la Chama cha Makandaraasi Wanawake Tanzania (TWCA) jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2024

Rais wa Chama cha Makandaraasi Wanawake Tanzania (TWCA), Judith Odunga akieleza jambo wakati wa Ufunguzi wa Kongamano la Nne la Chama hicho jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2024.




Baadhi ya washiriki wa Kongamano la Nne la Chama cha Makandaraasi Wanawake Tanzania (TWCA) wakimsikiliza Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour (hayupo pichani) wakati akifungua Kongamano hilo jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2024.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour akipokea zawadi kutoka kwa Rais wa Chama cha Makandaraasi Wanawake Tanzania (TWCA), Judith Odunga mara baada ya kufungua Kongamano la Nne la Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2024.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Balozi, Mhandisi Aisha Amour akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya Wahitimu wa Fani ya Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi kutoka Chuo Kikuu cha Mbeya (MUST) waliotunukiwa Vyeti vya kumaliza elimu yao mara baada ya kufungua Kongamano la Nne la Chama cha Makandarasi Wanawake Tanzania (TWCA) jijini Dar es Salaam, Oktoba 31, 2024.
PICHA NA WU


Na Mwandishi Wetu


Serikali imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa kuwawezesha wakandarasi wanawake kushiriki katika miradi mikubwa ya kimkakati, kuwapatia ujuzi na kuwahamashisha kufungua kampuni za ujenzi ili kushiriki kikamilifu katika kujenga Taifa.

Hayo yamebainishwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Ujenzi, Balozi Mhandisi, Aisha Amour, wakati akifungua Kongamano la nne la wanawake wakandarasi Tanzania ambalo limefanyika Oktoba 31, 2024 mkoani Dar es Salaam, huku akisisitiza wanataaluma hao kuendelea kushikamana kwa kuchangamakia fursa zinazojitokeza.

Amesema serikali itaendelea kufanyia kazi changamoto zote za makandarasi wa ndani ikiwemo wanawake, na kwamba jambo ambalo limekuwa likiwakwaza wengi ni kipaumbele cha kisheria ambapo vipengele vyake vingi vimerekebishwa kwa kupunguza masharti ikiwemo kuongezwa kiwango cha gharama ya miradi kutoka Sh. Bilioni 10 hadi 50.

“Serikali inaendelea na mikakati ya kukuza na kuwainua wazawa hasa kupitia Mabadiliko ya sheria ya manunuzi, hivyo tunaomba mjitokeze kuomba kazi katika zabuni mbalimbali za ujenzi zinazotangazwa”, amesema Balozi Amour

Ameongeza kuwa katika juhudi za kuwajengea uwezo Wakandarasi wanawake wazawa Serikali ya Awamu ya Sita kupitia Wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2024/25 imetenga miradi ya ujenzi wa barabara yenye urefu wa jumla ya kilometa 20 ambayo itatekelezwa mkoani Songwe na makandarasi wanawake ikiwa ni juhudi ya serikali kuendelea kuwajengea uwezo.

Ameeleza pia Wizara hiyo kupitia Kitengo chake cha Ushirikishwaji wa Wanawake katika kazi za barabara imekuwa ikitoa mafunzo maalum kwa wanawake na vikundi vya wanawake na kusisitiza kuwa hadi sasa wanawake 574 wenye Kampuni za ukandarasi na walio katika vikundi mbalimbali wamepatiwa mafunzo.

“Mafunzo haya ni moja ya mikakati ya Serikali ya kuwajengea uwezo wanawake kwa kuwapatia ujuzi na kuwahamasisha kufungua kampuni za ujenzi na matengenezo ya barabara hususani za Teknolojia Stahiki ya Nguvukazi ambapo kwa mwaka huu wa fedha, mafunzo yamefanyika jijini Tanga huku jumla ya washiriki 30 kutoka mikoa mbalimbali wakipatiwa mafunzo”, amefafanua Katibu Mkuu

Kwa upande wake, Rais wa Chama cha Wanawake Makandarasi Tanzania (TWCA) Judith Odunga, amesema chama hicho kimepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kuongeza wanachama hai 300, kuweka uhusiano mzuri na taasisi za kifedha kama NMB na CRDB, hali inayowasaidia kupata mikopo ya mtaji kwa kutumia mkataba wa mradi husika kama dhamana.

Pia amesema kwa sasa chama hicho kimewezesha mafunzo ya wanachama wake ikiwemo ya usimamizi wa mikataba, miradi na utafutaji wa masoko, huku akieleza kuwa imesaidia kuongeza kazi za ujenzi wa barabara zilizotengwa kwa ajili ya wanawake.

“Miradi mikubwa kwa wanawake kwa mara ya kwanza imetangazwa yenye urefu wa kilomita 20 kwa kiwango cha lami chini ya Wizara ya Ujenzi, jambo hili halijawahi kutokea, ni miradi ambayo baada ya kiongozi wetu kuipigia kelele serikali na kuiomba, Rais Samia Suluhu Hassan amehakikisha jambo hilo limetekelezeka,” amesema Judith.

Mafanikio mengine amesema kuwa ni baadhi ya kero za kodi kupatiwa ufumbuzi na zingie zinaendelea kutafutiwa suluhu, na kwamba Wakala wa Barabara Vijijini (TARURA) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) wamewatangazia kwamba wameandaa miradi mikakati ya kuwajengea uwezo wakandarasi wazawa.

No comments:

Post a Comment