Na Angela Msimbira, OR-TAMISEMI
NAIBU Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-TAMISEMI (Miundombinu), Mhandisi Rogatus Mativila amewaagiza Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha wanahamasisha uanzishwaji wa vituo vya kulelea Watoto Wadogo Mchana vya Kijamii katika vijiji/mtaa na kuwasilisha taarifa hii ifikapo Januari 30,2025
Mhandisi Mativila ametoa maagizo hayo leo Oktoba 4,2024, Jijini Dodoma alipomuwakilisha Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Adolf Ndunguru wakati akifungua mafunzo ya Kitaifa ya Uratibu na Utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya awali ya Mtoto kwa Maafisa ustawi wa Jamii wa Mikoa na Halmashauri.
Amesema kuwa katika kipindi hiki ukuaji na ujifunzaji wa watoto unakwenda kwa haraka sana huku mazingira yanayowazunguka yakiwa na mchango mkubwa wa kuamua hatima ya maisha yao, kivyo uwekezaji wa mapema katika huduma bora na kwa wakati kunawezesha kukuza rasilimali watu yenye tija kwa familia, jamii na taifa.
Amesema pia wahakikishe wanasimamia kwa ukamilifu Programu hii katika maeneo yao na taarifa za utekelezaji wa kila kipengele cha programu hii kuwezesha serikali kupata mafanikio na changamoto za Malezi na Makuzi ya watoto wa taifa hili.
Mhandisi Mativila amewataka kuendelea kutoa elimu kwa jamii kwa njia mbalimbali kuhusu umuhimu wa kuwekeza kwenye malezi bora ya watoto.
Aidha, amewataka kuhakikisha wanawatambua na kuendelea kushirikiana na wadau wote wa MMMAM waliopo kwenye mikoa na halmashauri ili kuchangia utekelezaji wa programu hiyo.
“Pia hakikisheni vikao vya mapitio ya Programu vinavyowaleta wadau kwenye ngazi ya mkoa na halmashauri vinafanyika kama vilivyoelekezwa na Programu hii.”amesisitiza
“Napenda kutoa rai kwenu mkawe mabalozi wazuri wa kuhakikisha watoto wadogo wenye umri wa miaka 0-8 wanapatiwa huduma zote za Malezi Jumuishi ikiwemo, Afya bora, Malezi yenye Mwitikio, Lishe toshelevu, Ujifunzaji wa Awali, na Ulinzi na Usalama wa Mtoto.
Naye, Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Chirdren in Crossfire Tanzania Craig Ferla amesema Uwekezaji wenye tija kwa watoto walio chini ya miaka 0-8 nchini kutasaidia kuchagiza nguvukazi ya maendeleo katika vizazi vijavyo hivyo jamii haina budi kuhakikisha inatumia muda kuwekeza kwenye makuzi ya mtoto ili kupata taifa lenye tija.
Aidha, amewataka Maafisa Ustawi wa Jamii kuhakikisha wanatumia ujuzi, akili na maarifa waliyoyapata katika mafunzo hayo katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa jamii ili kupata watoto wenye malezi, makuzi na maendeleo yatakayosaidia Jamii na Taifa kwa ujumla
No comments:
Post a Comment