Na WMJJWM, Dar Es Salaam
Kuelekea maadhimisho ya Siku ya mtoto wa kike Oktoba 11, 2024 Mamlaka za Serikali za Mitaa zimeshauriwa kuhakikisha hamasa inatolewa kwa watoto wa kike kushiriki katika uchaguzi kwa kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwenye majukwaa yao katika ngazi za shule na kwenye jamii.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju ametoa rai hiyo Oktoba 02, 2024 jijini Dar Ea Salaam wakati akizungumza na waandishi wa Habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike Oktoba 11, 2024.
Mpanju amebainisha kwamba, Serikali inaratibu uanzishwaji wa majukwaa mahsusi kwa ajili ya kuwajengea uwezo watoto shuleni kwa usaidizi wa walimu wa malezi na unasihi ili kukabiliana na ukatili unaoweza kutokea nyumbani, barabarani na shuleni, ambapo kufikia Septemba, 2024 jumla ya madawati 3,618 yameundwa, kati ya hayo 2,471 katika shule za msingi na 1,147 katika shule za sekondari.
Amesema, Kaulimbiu ya maadhimisho kwa mwaka huu ni "Mtoto wa Kike na Uongozi; Tumshirikishe, Wakati ni Sasa" ambayo, inahimiza uhamasishwaji wa mtoto wa kike kushiriki katika kugombea nafasi za uongozi kwenye chaguzi zote kwa umri wake ili ajifunze na apate stadi za uongozi kwa lengo la kumuandaa kuwa kiongozi wa sasa na siku za baadaye.
"Kwa mujibu wa takwimu za Sensa ya Watu na Makazi za mwaka 2022, idadi ya watoto kwa Tanzania Bara ni milioni 29,365,234 ambapo kati yao watoto wa kike ni milioni 14,680,895 sawa na nusu ya watoto wote nchini. Kundi hili hili la watoto wa kike linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na vitendo vya ubakaji, ulawiti, mimba na ndoa za utotoni." amesema Mpanju.
Ameongeza kuwa, Taarifa ya makosa ya Ukatili wa Kijinsia na Unyanyasaji za Jeshi la Polisi kwa kipindi cha Januari hadi Desemba, 2023 inaonyesha kuwa matukio ya ukatili dhidi ya watoto yalikuwa 15,301 ukilinganishwa na matukio 12,163 kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 25.8 hivyo jamii na wadau hainabudi kuunganisha nguvu katika kumlinda mtoto hasa wa kike.
Ametaja mikoa ya Kipolisi iliyokuwa na takwimu za juu za ukatili wa watoto ni Arusha matukio 1089, Morogoro 976, Tanga 884, Kinondoni 789 na Mjini Magharibi 788 matukio. Makosa yenye idadi kubwa ya waathirika ni kubaka (8,185), kulawiti (2,382), kumpa mimba mwanafunzi (1,437), kumzorotesha mwanafunzi (922) na shambulio la aibu (396).
Vilevile Mpanju ameweka wazi sababu za malezi duni kwa watoto, kwa mujibu wa taarifa ya Utafiti wa Hali ya Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria nchini ya mwaka 2022, kuwa mifarakano na migogoro katika familia, ilipelekea watoto hao kuanza ngono katika umri mdogo hivyo kuchochea mimba za utotoni.
Rebecca Gyumi kutoka taasisi ya Msichana Initiatives akizungumza kwa niaba ya wadau wa kutetea mtoto wa kike, amesema kama wadau wako tayari kuendelea kutekeleza afua mbalimbali za kumlimda mtoto wa kike kama zinavyoelekezwa na Serikali.
Maadhimisho hayo ni tamko la Mkutano Mkuu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa la tarehe 19 Desemba 2011. Lengo la maadhimisho hayo ni kutambua changamoto za kipekee anazokutana nazo mtoto wa kike zinazomnyima haki yake ya msingi ya kukua na kufikia ukuaji uliotimilika.
No comments:
Post a Comment