
Na Okuly Julius _Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri qMkuu (Sera Bunge na Uratibu), Mhe Ummy Nderiananga amesema Sera, Sheria na Miongozo ya Maafa ni lazima isimamiwe na kutekelezwa kikamilifu kwani ndiyo njia pekee ya kupunguza madhara ya maafa.
Amesema kama kuna ulazima wa kuhamisha watu wanaoishi katika maeneo hatarishi hususani mabondeni na kuwapeleka katika sehemu salama za miinuko, suala hilo ni halina budi kutekelezwa ipasavyo.
Nderiananga ametoa kauli hiyo leo Oktoba 7,2024 jijini Dodoma wakati akifungua mafunzo ya usimamizi wa maafa kwa waratibu wa maafa wa wizara na taasisi, mashirika ya umoja wa mataifa na kimataifa na asasi za kiraia
"hatuna budi kuendelea kuhifadhi mazingira ikiwemo misitu ya asili na vyanzo vya maji; kuendelea kutoa elimu ya maafa katika jamii ili wananchi waelewe masuala ya usimamizi wa maafa na nini wanatakiwa kufanya ili kupunguza athari za maafa katika meneo yao, "ameeleza Nderiananga
Amesema Matukio ya Maafa yanayosababishwa na majanga ya asili na yale yanayotokana na shughuli za kibinadamu yamekuwa yakiongezeka.
Ambapo Maafa hayo pamoja na kuathiri maisha ya watu na mali zao, yamekuwa yakileta madhara makubwa ya kijamii na kiuchumi kwa eneo husika na nchi kwa ujumla na kurudisha nyuma hatua ya maendeleo ambayo imeishafikiwa kwa muda mrefu.
Naibu Waziri wa huyo ameongeza kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau kwa kipindi cha mwaka 2020 - 2024 imeendelea kutoa kipaumbele katika usimamizi wa maafa ambapo miongoni mwa hatua zilizochukukuliwa ni kutunga Sheria mpya na kuandaa miongozo ya usimamizi wa Maafa,
kuendesha mazoezi ya mezani ya nadharia ya kujiandaa na kukabiliana na maafa kwa majanga ya mafuriko, vimbunga na tsunami, kuimarisha maghala ya kuhifadhi vifaa vya msaada katika kanda sita kwa kuongeza vifaa vya kutolea huduma za kibinadamu.
Pia, kutoa vifaa vya misaada ya kibinadamu kwa wananchi walioathirika na maafa katika Halmashauri mbalimbali nchini, kufanya mafunzo kwa kamati za usimamizi wa maafa za mikoa na wilaya na voluntia.
Ikiwemo pia kutoa elimu kwa umma, wataalam wanaosimamia asasi za kiraia na waandishi wa habari kutoka katika redio za kijamii nchini kuhusu masuala ya usimamizi wa maafa.
Kuandaa Mipango ya Wilaya ya Kujiandaa na Kukabili Maafa na Mikakati ya kupunguza Vihatarishi vya Maafa.
Kuanzisha Chumba cha Kufuatilia Mwenendo wa Majanga na Utoaji wa Tahadhari za Mapema katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura chenye vifaa vya TEHAMA pamoja na mifumo ya kufuatilia mwenendo wa majanga na kufanya tathmini ya hali ya uwezekano wa kuathirika ili kutoa tahadhari kwa wakati kwa ajili ya jamii husika kuchukua hatua.
Kuanza na kuendelea na ujenzi wa Kituo cha Taifa cha Usimamizi wa Maafa katika eneo la Nzuguni B, lililopo Dodoma ambapo ujenzi kwa awamu ya kwanza unajumuisha maghala wawili umekamilika na awamu ya pili inayohusisha jengo la utawala inaendelea.
Pamoja na kuimarisha uwezo wa vifaa vya kukabiliana na maafa na maokozi kwa kununua boti na kuwezesha vikundi vya wavuvi katika bahari ya Hindi na Ziwa Viktoria.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanahudhuriwa na washiriki wapatao 100, ikiwa ni sehemu ya waratibu wa maafa waliopata fursa hivyo kutakiwa kuwa mabalozi wa kupeleka ujuzi watakaopata kwa wataalam wengine.




No comments:
Post a Comment