WANANCHI WAKUBALI YAISHE, BANGI KUBAKI HISTORIA TARIME - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, October 9, 2024

WANANCHI WAKUBALI YAISHE, BANGI KUBAKI HISTORIA TARIME

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama ikiwemo jeshi la polisi, jeshi la akiba pamoja na wananchi imefanya operesheni kubwa ya kihistoria kwa muda wa wiki tatu katika wilaya ya Tarime na Serengeti, mkoani Mara kwa lengo la kukabiliana na tatizo la uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, hususan bangi.

Operesheni hiyo imefanyika katika vijiji vya  Matongo, Nyarwana, na Weigita vilivyopo bonde la Masinki, pia vijiji vya  Nkerege, Kembwe, Nyakunguru na Iseresere pamoja na eneo la bonde la mto Mara. 

Akizungumza mara baada ya operesheni hiyo  tarehe 8 Oktoba, 2024 Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Aretas Lyimo amesema, jumla ya ekari 3,007.5 za mashamba ya  bangi  zimeteketezwa katika operesheni hiyo. Aidha, kilogramu 7,832.5  za bangi kavu, na kilogramu 452 za mbegu za bangi  zilikamatwa, ambapo watuhumiwa 17 walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.

Kamishna Lyimo amesema operesheni hii ni sehemu ya jitihada za serikali kulinda jamii dhidi ya madhara ya dawa za kulevya na amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu shughuli zinazohusiana na dawa hizo.


Mamlaka imebaini kuwa, kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani ambao huwapa mitaji wakulima wa Tarime kisha bangi ikishakomaa huvunwa na kusafirishwa kwenda  kuuzwa. 

“Tunatoa miezi mitatu kwa wananchi wa mkoa wa Mara kuhakikisha wanaacha kabisa kujihusisha na kilimo cha bangi. Baada ya muda huo, tutafanya operesheni kubwa kwa namnna nyingine na kuhakikisha maeneo haya yanabadilishiwa matumizi na hayatumiki tena kwa kilimo cha  bangi. Pia wote wanaotetea uhalifu huu watachukuliwa hatua ili kuhakikisha wanachi wote wanatii sheria za nchi” 

Aidha, Mkuu wa wilaya ya Tarime Mhe. Meja Edward Gowele amekiri wilaya yake kukabiliwa na changamoto ya kilimo cha bangi hususan katika eneo la bonde la mto Mara na tayari serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hiyo.


“Tumeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya bangi na hasara wanayoweza kuipata kwa kujihusisha na kilimo cha bangi na walio wengi wametuahidi kuachana na kilimo cha bangi”


Kwa upande wake Mwita Mataro afisa wa maji kutoka bodi ya maji bonde la ziwa victoria dakio la Mara ambaye pia ni msimamizi wa rasilimali za maji katika mkoa wa Mara amesema lengo kubwa la bodi ni kuhakikisha rasilimali za maji zinatunzwa na kuendelezwa pasipo kuruhusu uharibifu wa aina yoyote.

“Tumejionea hali halisi ya bonde na tumeshuhudia zao la bangi likiwa limelimwa katika bonde la mto Mara. Sheria za rasilimali za maji haziruhusu kilimo haramu cha zao la bangi. Hata mazao mengine halali yanapaswa kulimwa umbali wa mita 60 kutoka mtoni. Hao wanaolima bangi ni sehemu ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji kwa sababu mwisho wa siku huu udongo wote mvua zitakaponyesha tope lote linatiririkka kwenda kwenye mto’’ amesema Mataro.
Ameongeza kuwa , Bodi hiyo imeandaa mpango kwa kidakio cha Kaskazini ambao unataja shughuli gani zinatakiwa kufanyika kwenye vyanzo vya maji ambazo ni rafiki, na wao kama bodi watasimamia kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa na hifadhi ya maji inalindwa.

Naye Lepapa Molel afisa kilimo kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mara amesema wakulima wengi wanalima bangi kwa kutegemea maji yanayotoka mto Mara “Nashauri wakulima wageuke na kuanza kulima mazao ya chakula yanayoweza kuwapa chakula na fedha  kuliko bangi”.                 

Wanakijiji wafyeka bangi yao wao wenyewe

Katika hali isiyotarajiwa wananchi wa kijiji cha Nkerege kata ya Kiore wilayani Tarime Mara waliamua kushirikiana na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya katika zoezi la kufyeka na kuteketeza mashamba ya bangi ili kuleta hali ya amani na utulivu kijijini hapo. Uamuzi huo ulitokana na hofu iliyojitokeza wakati wa operesheni ya kuondoa bangi, ambapo watu walikimbia makazi yao wakihofia kukamatwa  jambo lililoathiri shughuli zao za kijamii na kiuchumi.

Akizungummzia sakata hilo ,  diwani wa kata ya kiore Rhobi John alieleza kwamba wananchi wa Nkerege kwa kauli moja wameikataa bangi na kilimo hicho hakitalimwa tena kijijini hapo.
“Jana usiku wakina baba, wakina mama na vijana wote wameamua bangi haitaonekana tena, yaani sisi wenyewe tutakuwa walinzi sisi kwa sisi. Unapoona wenzako analima ni lazima kufuatilia na kutoa taarifa. Naishukuru cabinet ya wanasheria kutoka Mamlaka  kutoa elimu, akina mama na vijana waliikuwa hawajapata elimu na walidhani hili ni zao bora kwao”alisema 

Mzee Julius Zakaria Matiku, mwenyekiti wa mila katika ukoo wa Wasweta, alisema, "Tumekubaliana kuteketeza bangi ili kuondoa tatizo hili la kukimbiakimbia. Kijana atakayekamatwa akilima bangi, nitalipiza faini ya ng'ombe watano." Aliongeza kuwa mzee wa mila ana jukumu la kuhakikisha kuwa sheria zinaheshimiwa katika kijiji.

Kadhalika, katibu wa mila Burima Marwa Nyawise alisema kama wazee, wameamua kuteteketeza bangi ili waweze kulima mazao mengine kama mahindi, ufuta na kuendelea kufuga mifugo yao katika pori hilo. " Pori hili ni safi kwa kulima kitu chochote kama vile mahindi maharage ufuta vinakubali. Kwahiyo, hili zao la bangi limetutosha. Sasa watoto watulie nyumbani, wanawake wapikie watoto. Sisi malengo yetu ya kuja humu ni kuhakikisha tumeliteketeza hili zao la bangi" alisema. 

Mamlaka ya Kudhiitia Kupambana na Dawa za Kulevya inaendelea kufanya operesheni nchi nzima ili kuhakiksha dawa za kulevya za mashambani na viwandani zinatokomea na Tanzania inakuwa huru dhidi ya dawa za kulevya. Hivyo, ni jukumu la kila mmoja kupiga vita dawa za kulevya. Tusikubali kuwa sehemu ya kuangamiza taifa letu kwa kuendelea kulima na kufanya biashara ya dawa za kulevya


No comments:

Post a Comment