ZAIDI YA BIL.300 ZIMETUMIKA KUWEKEZA KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI YA HALMASHAURI NCHINI - CHEYO - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, October 10, 2024

ZAIDI YA BIL.300 ZIMETUMIKA KUWEKEZA KWENYE MIRADI YA KIMKAKATI YA HALMASHAURI NCHINI - CHEYO


Na. Asila Twaha OR -TAMISEMI, Dodoma


Mkurugenzi wa Idara ya Sera na Mipango Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Bw. John Cheyo amesema kuanzia mwaka 2017/18 hadi sasa Serikali imeshatoa zaidi ya Sh. Bil. 300 kwa ajili ya kuwekeza katika miradi ya kimkakati inayotekelezwa kwenye Halmashauri nchini.

Amesema Ruzuku hiyo inatolewa na Serikali kwa ajili ya kutekekeza miradi ya kuongeza mapato katika Mamlaka za Serikali za Mitaa kama vile uwekezaji wa ujenzi wa stendi ya Magufuli katika Manispaa ya Ubungo.

Bw. John Cheyo ameyasema hayo leo Oktoba 10, 2024 mkoani Dodoma wakati akifungua mafunzo kwa Makatibu Tawala Wasaidizi wa Idara ya Mipango na Uratibu katika Mikoa, Wakuu wa Idara za Mipango na Uratibu, Vitengo vya Fedha na Sheria wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhusu matumizi ya Mwongozo wa Uanzishwaji na Usimamizi wa Kampuni Mahsusi za Uendeshaji wa Miradi ya Vitega Uchumi kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“waataalamu tuliopewa dhamana tuwashauri viongozi wetu kwa kuanzisha miradi yenye kuleta tija kwasababu wananchi wakiona miradi wanategemea kupata huduma bora” amesema Cheyo.

Aidha, Bw. Cheyo amesema, Serikali ilitafuta fedha na kuzielekeza kwenye Halmashauri kuangalia fursa zilizopo ili kuanzisha miradi ya kimkakati inayoweza kutekelezwa katika Halmashuri zao na kuwa chanzo cha mapato kitakachoweza kuzisaidia Halmashauri kwa kuongeza ukusanyaji wa mapato lakini pia kupeleka huduma bora kwa wananchi pasina kusubiri fedha kutoka Serikali Kuu.

Bw. Johson Nyingi Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tawala za Mikoa, Ofisi ya Rais – TAMISEMI amesema, lengo la mafunzo hayo ya siku mbili ni kujenga uelewa na kubadilishana uzoefu kuhusu taratibu za kuanzisha makapuni mahsusi kusimamia vitega uchumi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa na yatafanyika Mikoa na Halmashauri zote Tanzania Bara ambapo kwa sasa yameanza kwa Mikoa 9 na Halmashauri 16.

Naye Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mitaji ya Maendeleo Tanzania Peter Malika ameishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na kueleza kuendelea kuzisaidia Mamlaka za Serikali za Mitaa kupata fedha na kutoa mafunzo ili kuongeza wataalumu watakaoweza kusimamia miradi itakayoongeza kupata mapato katika Halamshauri.

Mafunzo kwa wataalamu hao yanayofanyika kwa muda wa siku mbili yanatolewa na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Mitaji (UNCDF).

No comments:

Post a Comment