BASHUNGWA ALINYOOSHEA KIDOLE BARAZA LA ARDHI KARAGWE, HAKI ITOLEWE KWA WAKATI. - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Wednesday, November 13, 2024

BASHUNGWA ALINYOOSHEA KIDOLE BARAZA LA ARDHI KARAGWE, HAKI ITOLEWE KWA WAKATI.


Waziri wa Ujenzi na Mbunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa ametoa wito kwa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuboresha utaoji huduma wa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya liweze kutenda haki kwa wakati katika usuluhishi wa migogoro na kupunguza malalamiko ya Wananchi ili kukomesha migogoro ya Ardhi Wilaya ya Karagwe.

Bashungwa ametoa rai hiyo leo Novemba 13, 2024 Wilayani Karagwe Mkoani Kagera katika Kikao cha Baraza la Madiwani cha kujadili taarifa za robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2024/25 kilichohusisha Watendaji wa Halmashauri na Kata.

“Mwenyekiti wa Halmashauri tutupie jicho na kuboresha Baraza la Ardhi ili kupunguza malalamiko ya wananchi, Mabaraza ya Ardhi yanapochelewesha haki kwa kumzungusha mwananchi ni gharama kubwa na yanatia umasikini”, amesema Bashungwa.

Ameitaka Halmashauri kufanya tathmini ya utoaji huduma wa Baraza hilo ili kujua changamoto zinazokwamisha utoaji wa haki kwa wakati na wanaohusika kukwamisha waweze kuchukuliwa hatua.

Bashungwa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kujikita katika mipango miji na upimaji wa ardhi katika maeneo yanayoendelea kukua ili kuendana na uwekezaji unaofanywa na Serikali katika miundombinu ili kuepusha migogoro ya ardhi kwa wananchi.

Aidha, Bashungwa ameitaka Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe kuweka mipango mahsusi na kufanya kampeni endelevu ya utunzaji wa mazingira kwa kupanda miti ya vivuli pamoja na matunda ili kusaidia utunzaji wa mazingira na vyanzo vya maji.

Kadhalika, Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi ina mpango wa kupeleka Kivuko katika Ziwa Burigi kitakachotoa huduma ya usafiri kwa wananchi wa Mirilo na Ruita katika Kata ya Rugu ili kuondokana na matumizi ya mitumbwi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Karagwe, Wallace Mashanda amewasisitiza Waheshimiwa Madiwani kuendelea na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo yanayowazunguka kwa kuendelea kupanda miti kwa wingi.



No comments:

Post a Comment