Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Awali na Msingi (BOOST) imewezesha mafunzo Walimu Wakuu 17,793 katika Mikoa 26 ya Tanzania Bara kuhusu uongozi na usimamizi wa Shule.
Hayo yamesemwa Novemba 06, 2024 mkoani Katavi na Mkurugenzi wa Elimu ya Awali na Msingi Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Abdul Maulid akizungumza katika halfa ya kuhitisha mafunzo hayo kitaifa ambapo amewataka walimu kusimamia ustawi na usalama wa wanafunzi shuleni.
‘’Walimu Wakuu ni nguzo muhimu katika sekta ya elimu, naamini mafunzo haya yatawasaidia kujenga mazingira bora ya kufundishia na kujifunza na kukuza vipaji vya wanafunzi’’ alisema Maulid.
Aidha ameongeza kuwa, kupitia BOOST Serikali imetumia zaidi ya Sh. Bilioni 230 kuwezesha ujenzi wa vyumba vya madarasa 7,230, matundu ya vyoo 11,297, majengo ya utawala 302 na nyumba za walimu 41’’ alibainisha Maulid.
Nae Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya awali na Msingi Ofisi ya Rais TAMISEMI Mwl. Suzan Nussu amesema inatarajia kuona shule zinaimarika kiutendaji hasa katika eneo la usimamizi na utoaji wa taaluma kwa ujumla, usimamizi na utekelezaji wa mtaala ulioboreshwa.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM) Dkt. Maulid J. Maulid, amesema mafunzo hayo yamewajengea uwezo Walimu Wakuu katika Uongozi na Usimamizi wa Shule pamoja na Utawala Bora kuhakikisha shughuli za ufundishaji na ujifunzaji shuleni zinafanyika kwa ubora na ufanisi unaotakiwa.
Wakizungumza kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa shule ya msingi Kasekese Mwl. Renatus Benson na Mwl. Shani Juma Mkuu shule ya msingi Itunya wameishukuru Serikali kuwapatia mafunzo walimu katika wilaya ya Tanganyika, ambapo wameahidi kuyatekeleza kikamilifu.
No comments:
Post a Comment