Na Okuly Julius_ Dodoma
SERIKALI imetoa kibali cha kuajiri walimu wa somo la biashara 4,000 kwa mwaka wa fedha 2024/25 kwa ajili ya kufundisha wanafunzi wa sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne kwa kufuata mtaala mpya unaotumika unaolenga kuleta mapinduzi ya elimu nchini kwa kuimarisha elimu ya biashara kwa wanafunzi.
Akifungua Mafunzo Elekezi ya siku tatu kwa Maofisa Uthibiti ubora wa Wilaya Wateule Jijini hapa jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda alisema, walimu hao watafundisha wanafunzi elimu ya biashara kuanzia mwakani.
“Katika mageuzi ya elimu, wanafunzi wanatakiwa kusoma somo la biashara kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne, ili kuhakikisha wanapata elimu hiyo muhimu ya mafunzo ya biashara na ndiyo maana Rais Samia ametoa kibali kuajiri walimu hao.
“Watoto lazima waanze kuandaliwa ili kuweza kujiamulia cha kufanya baada ya kumaliza kidato cha nne kwani watakuwa wamefundishwa mbinu za biashara zitakazowasaidia katika maisha yao, hata wakifeli kuendelea na masomo wanaweza kujiajiri."
Profesa Mkenda, aliwapongeza wathibiti ubora waliopenya kwenye chekecheke la kuwachuja, kwani hao waliopatikana wamepatikana kwa sifa na vigezo vinavyopimika kwani wana shahada ya uzamili, wana uzoefu na wana maadili na uwezo wa kufanya kazi vizuri.
Lakini pia aliwatia moyo wathibiti ubora 40 waliofeli katika mchujo huo, kwamba waombe kujiendeleza ili wawe na shahada ya uzamili na wizara ipo tayari kuwalipia na wakihitimu wataangaliwa.
Aliwaagiza wathibiti ubora hao wa wilaya wateule kwenda kufanya kazi kwa bidii katika kusimamia mageuzi katika sekta ya elimu kwa sababu wao ni jicho la wizara na ndiyo maana rais amewakubali na akakubali muundo wa uwepo wao katika halmashauri zote nchini, akawapa mishahara bora na stahili zao zote katika kutekeleza jukumu hilo la kuthibiti ubora wa elimu nchini.
Pia aliwataka wakatupie jicho kwenye tume ya watalaamu kutoka taasisi za elimu nchini ambayo inafanya kazi ya kuuinganisha mifumo wa kuwatambua wanafunzi kuanzia ngazi za elimu ya awali, vyuo vya kati na vyuo vikuu ili ajulikane amesoma wapi, chuo gani na anafanya nini sasa, lengo ni kuwa na mfumo bora wa takwimu za kujua wasomi wake wote nchini.
Pia aliwatakiwa kutupia jicho mageuzi ya elimu ya msingi ambayo yataanza mwaka 2027 kwa makundi mawili ya wanafunzi yatahitimu shule ya msingi; waliopo darasa la nne watahitimu darasa la saba mwaka huo na waliopo darasa la tatu watahatimu darasa la sita mwaka huo. Wakapohitimu wataingia kidato cha kwanza ambacho kitakuwa na mikondo mwili; mkondo elimu jumuishi na mkondo wa pili unaohusu elimu ya amali ambayo watajifunza ufundi mbalimbali ukiwemo michezo, muziki, kilimo, uvuvi, ufugaji, na ufundi mwingine.
Aliwataka wathibiti ubora hao kwenda kushirikiana na wakurugenzi wa halmashauri na walimu moja kwa moja kwa kuundi kundi la kuwaunganisha kwa ushirikiano huo watatambua kutambua changamoto zinazoweza kujitokeza na wajitahidi kutambua shule zote zilizopo katika halmashauri husika.
"jitahidini kutengeneza mtandao wenu na wakurugenzi na walimu ili muweze kutatua changamoto zinazoweza kujitokeza kwani kuna jambo linaweza kujitokeza na msifahamu ila kwa sababu mmeshatengeneza Mawasiliano mazuri lazima ujue mapema na kulifanyia kazi," alisema.
Pia wanaweza kutoa ushauri katika kuhakikisha maeneo mbalimbli ya kijiografia yanakuwa na shule za msingi na kama nafasi ni kubwa washauri shule za sekondari zijengwa na wasiote vipingamizi kama wananchi wamejenga jengo lakini hawana choo wasizuiliwe kuisajili na wathibiti wawashike mikono.
Pia alimwelekeza Mkurugenzi wa Wathibiti Wizara ya hiyo, Ubora Efraim Sembeye kuhakikisha anafanya msawazo wa wathibiti ubora kulingana na ukubwa wa eneo kusitokee eneo ambalo wathibiti ubora wamejazana kuliko eneo jingine na baadhi ya shule zenye walimu wakiume wote ziangaliwe kwani kuna watoto wa kike wanahitaji kusaidiwa na walimu wa Kike.
Naye Kaimu Katibu Mkuu, Michael John aliwapongeza wathibiti ubora 179 waliofika kwenye semina elekezi ya siku tatu na kuhakikisha wanakwenda kusimamia sera ya elimu 2014 toleo 2023 pamoja na utekelezaji wa mtaala mpya ambao katika maboresho ya muundo wa uwepo wao katika halmashauri zimeondolewa ofisi za kanda.
Akitua neno la shukrani Mwenyekiti wa Mkutano huo, Antipas Kayombo alisema, wathibiti ubora kutoka mikoa yote 26 watakwenda kutekeleza wajibu wao katika halmashauri mbalimbali nchini kwa kuzingatia sera, sheria, miongozo na kanuni walizopewa huku wakishirikiana na watendaji wengine katika halmashauri hizo.
No comments:
Post a Comment