Na Okuly Julius _ Dodoma
Serikali kupitia skolashipu ya ‘Samia Extended’ inalenga kusomesha vijana watano wa Kitanzania nje ya nchi katika ngazi ya Umahiri kwenye masuala ya Sayansi na Teknolojia ya Nyuklia.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda leo Novemba 7,2024, jijini Dodoma wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa jengo la maabara ya Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) zilizojengwa eneo la DungaZuze Zanzibar .
"Serikali, kwa kushirikiana na wadau, itaendelea kuongeza kiwango cha ufadhili kulingana na uwezo wa kibajeti,ili kuhakikisha kuwa nchi yetu inakuwa na wataalamu wa kutosha kati nyanja husika," ameeleza Prof. Mkenda
Aidha, Prof. Mkenda amesema uwepo wa Maabara Mpya ya Nguvu za Atomu upande wa Zanzibar ni hatua muhimu katika kuhakikisha matumizi ya teknolojia ya nyuklia yanakua na kuleta tija inayokusudiwa
“Matumizi ya maabara hizi pia yatasaidia kuongeza fursa za kufanya biashara na nchi nyingine kwa kuhakikisha usalama,” amesema.
Mkenda amesema maabara hizo zitakuwa msingi mzuri kwa shughuli za utafiti na mafunzo, zikiwawezesha wataalamu katika kufanikisha tafiti na miradi mbalimbali inayolenga kuboresha huduma na bidhaa katika sekta hizo muhimu.
“Aidha, uwepo wa maabara hii utaongeza uwezo wa kitaaluma wa wataalamu wetu, kuwezesha uhamishaji wa teknolojia,” amesema.
Amesema wizara yake kwa kushirikiana na Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania wamejenga ofisi na maabara hizo za nyuklia katika kanda nne ambazo ni Kanda ya Kaskazini (Arusha), Kanda ya Kati (Dodoma), Kanda ya Ziwa (Mwanza) na hivi karibuni watazindua Ofisi ya Zanzibar kwa lengo la kusogeza huduma kwa wananchi.
Amesema uzinduzi wa maabara na ofisi za tume hiyo zitakazozinduliwa hivi karibuni, zimejengwa eneo la DungaZuze Zanzibar, ambapo Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Hussein Ali Mwinyi atazindua Novemba 11, mwaka huu.
Amesema Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania, ilielekezwa kuhakikisha kuwa inaendelea kuimarisha huduma, tafiti na ubunifu unaolenga kuongeza wigo wa matumizi ya sayansi na teknolojia ya nyuklia katika sekta mbalimbali nchini.
Sambamba na hilo, hatua hiyo inalenga kusogeza huduma za uthibiti na kuhamasisha matumizi salama ya nyuklia karibu na wananchi wa Zanzibar.
Amesema teknolojia ya nyuklia ikitumika vizuri inaweza kuongeza tija katika sekta mbalimbali ikiwemo kuchunguza na kutibu ugonjwa wa saratani, kuboresha mbegu za mazao hasa yale ambayo yana ugumu kustawi na yanatoa mazao kidogo,
Pia kuua vimelea vinavyosabisha chakula kuharibika kudhibiti kuzaliana kwa wadudu wanaoeneza magonjwa kama vile mbung’o, kuhakiki uimara na ubora wa maungio ya matenki na mabomba makubwa ya mafuta au maji,
Kuhakiki ubora katika ujenzi wa barabara na reli, kusafisha maji taka kwa ajili ya kutumika katika shughuli nyingine, utafiti wa mafuta na gesi.
No comments:
Post a Comment