WAHITIMU VETA WAASWA KUUNDA VIKUNDI KUNUFAIKA NA MIKOPO YA SERIKALI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Saturday, November 22, 2025

WAHITIMU VETA WAASWA KUUNDA VIKUNDI KUNUFAIKA NA MIKOPO YA SERIKALI


Wahitimu wa Chuo cha Ufundi Stadi VETA Mikumi wamehimizwa kuunda vikundi na kuanzisha kampuni ili kunufaika na fursa za mikopo inayotolewa na Serikali pamoja na taasisi za kifedha nchini.

Wito huo ulitolewa na Mjumbe wa Bodi ya VETA, Abdulhamid Masai, aliyemwakilisha Mwenyekiti wa Bodi ya VETA, Prof. Sifuni Mchome, tarehe 20 Novemba 2025 wakati wa mahafali ya 28 ya chuo hicho.

Masai amesema kuwa Serikali imeweka mazingira rafiki kwa vijana kupata mikopo na mitaji kupitia Halmashauri na taasisi mbalimbali za kifedha, hivyo ni muhimu kwa wahitimu kushirikiana na kuunda vikundi ili kuongeza fursa za kufikiwa na huduma hizo.

“Serikalini na kwenye taasisi za kifedha kuna mikopo. Ni juu yetu vijana kuona namna ya kuungana na kunufaika na fursa hizo. Serikali ipo tayari kuwasaidia,” amesema Masai na kuongeza “Ukitaka kwenda haraka nenda peke yako, lakini ukitaka kufika mbali nenda na wenzako. Tokeni hapa kwa umoja anzisheni vikundi, fikirieni kuanzisha kampuni, na fanyeni kazi kwa ushirikiano,”

Aidha, amewahimiza wahitimu kutumia mikopo ya Halmashauri kusajili kampuni, kuanzisha biashara na kupata leseni zinazowawezesha kufanya kazi kwa weledi.

“Kama wewe ni fundi umeme ni vigumu kupata leseni bila kuwa chini ya kampuni. Jisajilini, jipangeni na muwe tayari kuanza kazi. Mmeshaingia kwenye hatua ya kujiajiri, kuajiriwa au hata kuwaajiri vijana wenzenu,” amefafanua.

Amebainisha kuwa, sambamba na kupata mikopo, kufanya kazi pamoja pia kunarahisisha kupata misaada mingine ya Serikali kama maeneo ya kufanyia kazi na ushauri wa kitaalam.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mikumi, Deusi Mbuge, amewahimiza wahitimu kuzingatia sheria, maadili na misingi ya jamii wanapoanza safari yao ya kujitegemea, huku wakitumia ujuzi walioupata kwa njia sahihi.

Amewakumbusha kutumia fusa za mikopo ya Halmashauri za Wilaya, miji na majiji kote nchini ambapo hutengwa asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo ikiwa ni asilimia 4 kwa vijana, 4 kwa wanawake na 2 kwa watu wenye mahitaji maalum.

Awali, Mkuu wa Chuo cha VETA Mikumi, Bi. Marynurce Kazosi, amesema jumla ya wanafunzi 271 wamehitimu katika ngazi mbalimbali, 172 wa ngazi ya pili na 99 wa ngazi ya tatu.

Amesema chuo kinaendelea kuchochea maendeleo ya jamii kupitia mafunzo yanayowahusu makundi yote ambapo mwa mwaka huu, chuo kimesajili wanafunzi 714 wa kozi ndefu katika fani 14 kuanzia ngazi ya kwanza hadi ya tatu, wakiwemo wanaume 420 na wanawake 294.

No comments:

Post a Comment