Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amekutana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, aliyefika Ikulu kujitambulisha, leo tarehe 22 Novemba 2025
Rais Dkt. Mwinyi amempongeza kwa kushika wadhifa huo na kumhakikishia ushirikiano wa kiwango cha juu katika utekelezaji wa masuala yanayohusu Muungano.
Dkt. Mwinyi amefahamisha kuwa mafanikio makubwa yamefikiwa katika kuzipatia ufumbuzi changamoto nyingi zilizokuwepo awali, hivyo juhudi zinapaswa kuendelezwa ili kuimarisha Muungano kwa maslahi ya pande zote mbili.
Naye Makamu wa Rais, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, amempongeza Rais Dkt. Mwinyi kwa ushindi mkubwa wa kuchaguliwa tena kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, na kuelezea matumaini yake ya kuiona Zanzibar ikifanya maendeleo makubwa zaidi katika miaka mitano ijayo.
Akizungumzia Muungano, ameahidi kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza dhamira thabiti ya kuufanya Muungano kuwa imara zaidi.




No comments:
Post a Comment