TEF YAMPONGEZA WAZIRI KUUNDA BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI - OKULY BLOG

Breaking

Music

Header ADS

Thursday, November 21, 2024

TEF YAMPONGEZA WAZIRI KUUNDA BODI YA ITHIBATI YA WAANDISHI WA HABARI


Na Mwandishi Wetu, JAB.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amempongeza Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Jerry William Silaa kwa kuunda Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari mapema mara baada ya kuteuliwa.

Balile amesema hiyo ni hatua kubwa kwani imechukua miaka Nane tangu kutungwa kwa Sheria ya Huduma za Habari Sura ya 229 inayotamka uundwaji wa bodi hiyo.

Ametoa kauli hiyo leo tarehe 21 Novemba, 2024 wakati akiwasilisha hoja za jukwaa hilo mbele ya Waziri kwenye Kikao cha kwanza cha kufahamiana na Wajumbe wa Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI) kilichofanyika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), jijini Dar es Salaam.

“Tunakushukuru sana Mheshimiwa kwa sababu imechukua miaka Nane tangu Sheria imepita 2016 na Bodi ilikuwa haijawahi kuundwa na leo tumesikia Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi Bw. Patrick Kipangula, siyo mgeni sana kwetu lakini leo tumemsikia kwa cheo kipya, tunashukuru sana na tunampongeza sana,” amesema Balile akionesha kuridhishwa na Hatua hiyo ya Waziri Silaa kuunda Bodi ya Ithibati.

Waziri Silaa aliiteua Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari Septemba 18 na kumteua Mwandishi wa Habari Nguli Tido Mhando kuwa Mwenyekiti wa Kwanza na wajumbe wengine sita kutoka Taasisi za Habari kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Huduma za Habari.

Wajumbe wa Bodi hiyo ni Bw. Thobias Makoba, Mgaya Kingoba, Dkt. Rose Reuben Mchomvu, Dkt Egbert Mkoko na Laslaus Komanya.



Akizungumza na Wadau wa Habari kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Uchaguzi Mkuu 2025, tarehe 19 Novemba, Waziri Silaa alibainisha kuwa uzinduzi rasmi wa bodi hiyo muhimu utafanyika mapema mwezi Disemba, 2024 na kwamba itafungua njia ya safari ya kuanzisha Baraza Huru la Habari na pia Mfuko wa Mafunzo kwa Wanahabari na tathimini ya hali ya uchumi kwa vyombo vya habari.

Katika hoja yake Balile alimuomba Waziri kuwa na kikao kazi kitakachogusia Sera ya Habari, Sheria na mfuko wa mafunzo ili kupata uelewa wa pamoja wa namna ya kuiboresha tasnia ya Habari na Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Ombi kama hilo pia liliwasilishwa na Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura aliyemuomba Waziri katika vikao vijavyo kuwa na majadiliano ya namna Baraza Huru la Habari lililoundwa na Sheria ya Huduma za Habari litakavyoendesha majukumu yake ili kujitofautisha na Baraza la Habari Tanzania (MCT) ili kuondoa mgongano.



Picha ya pamoja

No comments:

Post a Comment